TIMU ya Taifa ya Wanawake, Twiga Stars ipo kazini inapambania nembo ya taifa kwa kupata ushindi katika viunga vya Azam Complex kwenye mechi ya kwanza ya raundi ya pili ya michuano ya kuwania Fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Wafcon) 2024.
Ni dhidi ya Togo kwenye Uwanja wa Azam Complex, jijini Dar ambapo wameanza kwa kasi wakishinda kwa mabao matatu Twigas Stars ambayo nahodha ni Opag Clement.
Twiga Stars kwa ushindi kwenye mchezo huu wa nyumbani inajitengenezea mazingira mazuri kwa mchezo wa marudiano utakaopigwa Desemba 5, ili kufuzu kwenda Morocco.
Timu hiyo ilianza safari ya kwanza kwa kupokea kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa Ivory Coast ugenini na kisha kumaliza kazi Azam Complex kwa ushindi wa mabao 2-0 na kuvuka kwa mikwaju ya penalti 4-2, wakati Togo ilianza kwa kuing’oa Djibouti kwa jumla ya mabao 13-0, ikishinda kwanza kwa 7-0 kisha 6-0.
Miongoni mwa nyota wa Twiga Stars ni pamoja na Fatma Issa maarufu kama Fetty Densa ambaye aliweka wazi kuwa malengo ni kupata ushindi kwenye kila mchezo.