SIMBA YAYEYUSHA DAKIKA 450 BILA USHINDI

WAWAKILISHI wa Tanzania kwenye Ligi ya Mabingwa, Simba wameandika rekodi yao kwenye anga hilo kwa kukomba dakika 450 sawa na mechi tano bila kuambulia ushindi.

Kwenye mechi hizo, mbili ilikuwa ni African Football League, (AFL) na tatu Ligi ya Mabingwa Afrika. Katika mechi tano, tatu wamecheza nyumbani na mbili ugenini.

Katika mechi za AFL, ilikuwa hivi; Simba 2-2 Al Ahly na Al Ahly 1-1 Simba. Simba iligotea hatua ya robo fainali kwa kanuni ya bao la ugenini.
Kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, mechi ya kwanza ilikuwa Power Dynamos 2-2 Simba na Simba 1-1 Power Dynamos. Ni faida ya mabao ya ugenini yaliwapa fursa Simba kutinga hatua ya makundi.

Mchezo wa kwanza hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika ambao unakamilisha dakika 450, ilikuwa Simba 1-1 ASEC Mimosas.

Mechi tano mabao ya kufunga ni 7 sawa na yale waliyofungwa. Hivyo Simba kufunga kimataifa ni kawaida yao na kufungwa pia ni kawaida yao.