KIMATAIFA kazi inakwenda kuanza kwa wawakilishi wa Tanzania Simba na Yanga kufanya kweli katika Ligi ya Mabingwa Afrika. Muda ni sasa kwa wachezaji kufanya kweli katika mechi zote za nyumbani na ugenini.
Katika hatua ya makundi ni msako wa pointi tatu hivyo hesabu za kufikia hatua ya robo fainali zinaanza kupangwa sasa. Ni muda wa kufanya kweli kimataifa kwa kufuta makosa yaliyopita.
Yanga chini ya Kocha Mkuu, Miguel Gamondi inakibarua cha kuanzia ugenini huku Simba wao kete yao ya kwanza itakuwa nyumbani dhidi ya ASEC Mimosas, Novemba 25. Hapa tunakuletea baadhi ya mambo yanayopaswa kufanyiwa kazi namna hii:-
Ulinzi
Kwa timu zote mbili ambazo zinaipeperusha bendera ya Tanzania muhimu kuongeza umakini kwenye ulinzi. Ipo wazi kwamba Yanga kwenye ligi ya ndani wamekuwa imara hata katika Ligi ya Mabingwa Afrika.
Ikumbukwe kwamba kwenye mechi mbili dhidi ya ASAS Uwanja wa Azam Complex ni bao moja walifungwa. Katika mchezo dhidi ya Al Merrikh kwenye mechi mbili ambazo ni dakika 180 hawakufungwa.
Kwa upande wa Simba kwenye ligi ya ndani ukuta umekuwa na shida kwa kuruhusu mabao mengi ambayo ni 11. Shida hiyo haipo ndani bali hadi Ligi ya Mabingwa Afrika. Kwenye mchezo dhidi ya Power Dynamo ni mabao matatu walifungwa sawa nay ale ambayo safu ya ushambuliaji ilifunga.
Ushambuliaji
Safu ya ushambuliaji ya Yanga kasi yake kubwa ni kwenye kuwatumia viungo kutengeneza mabao mengi. Katika Ligi ya Mabingwa Afrika ni muhimu kasi hiyo kuendelea. Katika mechi nne za Ligi ya Mabingwa Afrika Yanga ilifunga jumla ya mabao 10 idadi ambayo si haba ikiendelea namna hii furaha itazidi mitaa ya Jangwani.
Simba ni mechi mbili pekee walizocheza dhidi ya Power Dynamos na walifunga mabao matatu kupitia kwa kiungo Clatous Chama aliyefunga mabao mawili na bao moja lilikuwa la kujifunga.
Kwa upande wa Simba wanakazi kubwa kufanyia kazi makosa kwenye mechi zilizopita kutokana na kuwa na uwezo wa kutengeneza nafasi kisha kuzitumia inakuwa ni tatizo.
Mechi za nyumbani
Kwenye mashindano ya kimataifa kila mmoja anajivunia kwenye mechi za nyumbani. Yanga wanakumbuka kwamba kwenye fainali dhidi ya USM Alger ya Kombe la Shirikisho Afrika kete ya nyumbani ilichangwa vibaya.
Katika fainali ya kwanza iliyochezwa Uwanja wa Mkapa ubao ulisoma Yanga 1-2 USM Alger na walipokwenda ugenini ilikuwa USM Alger 0-1 Yanga walishindwa kutwaa ubingwa kutokana na faida ya mabao ya ugenini ambayo ilikuwa kwa USM Alger.
Mchezo wa kwanza kwa Yanga katika hatua ya makundi unatarajiwa kuwa ugenini dhidi ya CR Belouizdad Novemba 24 hivyo kete yao ya nyumbani dhidi ya Al Ahly wana kazi ya kupambana kupata ushindi.
Simba wanakumbuka kwenye African Footbal League waliishia hatua ya robo fainali kwa kushindwa kumaliza kete ya kwanza nyumbani waliporuhusu kufungana mabao 2-2 Al Ahly. Kete yao ya kwanza itakuwa nyumbani dhidi ya ASEC Mimosas hivyo makosa yao wanapaswa wayafanyie kazi.
Rekodi
Rekodi kwa wawakilishi hawa wa Tanzania zinatafuta ambapo Yanga inatafuta rekodi ya kutinga hatua ya robo fainali huku watani zao wa jadi rekodi yao wanayoitafuta ni kujinasua kutoka kwenye hatua ya makundi na kufikia nusu fainali kwa kuwa hatua ya robo fainali hata msimu uliopita walikuwa hapo.
Imeandikwa na Dizo Click na kutoka gazeti la Championi Jumatano.