FELIX MINZIRO APEWA MKONO WA ASANTE

RASMI Tanzania Prisons imeachana na aliyekuwa kocha mkuu wa timu hiyo, Freddy Felix Kataraiya Minziro kufuatia matokeo yasiyoridhisha na sasa Maafande hao watabaki chini ya msaidizi, Shaban Mtupa.

Minziro alijiunga na Wajelajela hao mapema msimu huu ambapo ameiongoza mechi tisa za mashindano ya Ligi Kuu akishinda mechi moja, sare nne na kupoteza minne na kuwa nafasi ya 14 kwa pointi saba.

Hata hivyo katika mechi tisa alizosimamia Minziro ni mchezo mmoja pekee ambao hawakuruhusu bao ikiwa ni dhidi ya Singida Fountain Gate ulioisha kwa suluhu ya bila kufungana na kufanya Prisons kuwa miongoni mwa timu mbili zilizofungwa idadi kubwa ya mabao (15) ikiachwa moja na Mtibwa Sugar.

Taarifa iliyotolewa na uongozi wa timu hiyo umemshukuru kocha huyo kwa kipindi chote alichoitumikia huku ukieleza kuwa kwa sasa Mtupa ndiye atasimama hadi pale watakapopata wa kukabidhiwa majukumu.

Kocha huyo aliibuka ndani ya Tanzania Prisons akitokea Klabu ya Geita Gold ambayo kwa sasa inanolewa na Kocha Mkuu Hemed Morocco.