YANGA YAPENYA TANO CAF TIMU BORA

KLABU ya Yanga imetinga hatua ya tano bora kuwania tuzo ya klabu bora kwa wanaume kutoka CAF kwa mwaka 2023.

Ikumbukwe kwamba Yanga kwenye Kombe la Shirikisho Afrika 2022/23 waligotea nafasi ya pili na katika ligi ya ndani walitwaa taji la Ligi Kuu Bara.

Zama hizo ilikuwa inanolewa na Kocha Mkuu, Nasreddine Nabi na kwa sasa ipo chini ya Kocha Mkuu Miguel Gamondi.

Awali zilikuwa zinawania timu 10 ambazo ni Al Ahly ya Misri, Wydad na Raja Casablanca kutoka Morocco, Mamelodi Sundowns na Marumo Gallants kutoka Afrika Kusini, Esperance de Tunisia, USM Alger na CR Belouizdad kutoka Algeria, Asec Mimosa ya Ivory Coast na Tanzania ikiwakilishwa na Yanga.

Tuzo hizo zitatolewa Desemba 11 nchini Morocco ambapo timu zilizotinga tano bora ukianza na Yanga kuna USM Alger, Al Ahly, Waydad na Mamelod.