YANGA WABADILI HESABU, MIPANGO IPO HIVI SASA

Kocha Mkuu Yanga, Miguel Gamondi ameweka wazi kuwa hesabu zake kwenye anga la kimataifa kwa ajili ya mechi  za Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya CR Belouzdad inayonolewa na  Mbrazili Marcos Paqueta aliyechukua nafasi ya Sven Vandebroeck zimeanza sasa.

Sven kwa sasa ni kocha huru ambapo anatajwa kwamba yupo kwenye hesabu za kurejea ndani ya kikosi cha Simba.

Yanga ni vinara kwenye ligi wana pointi 24 baada ya kucheza mechi tisa,  ushindi ni mechi nane na kupoteza moja dhidi ya Ihefu, imepangwa Kundi D katika michuano  ya CAF ikiwa na Al Ahly ya Misri, CR Belouzdad ya Algeria na Medeama ya Ghana.

Gamondi amesema ubora wa kikosi chake unatokana na mambo mengi huku akitaja kuwajibika kwa kila mmoja kuwa ndio siri kubwa ya mafanikio waliyonayo.

Yanga kuanzia benchi la ufundi, wachezaji na viongozi tumekuwa wamoja hii ni njia bora na ya kujenga pamoja ili kuweza kufikia mafanikio jambo ambalo hadi tulipofikia sasa tunaona mwanga,” amesema Gamondi na kuongeza;

“Akili yote sasa imehamia kimataifa tunataka kuweka rekodi nyingine baada ya kutinga hatua ya makundi baada ya miaka 25 malengo sasa ni kusonga mbele zaidi kwa kucheza robo fainali.”

Yanga imetinga makundi ikiwa ni miaka 25 tangu ilipofika hatua hiyo kwa mara ya kwanza mwaka 1998, ikiwa ni miezi michache baada ya fainali ya Kombe la Shirikisho.