Mshambuliaji wa Timu ya Taifa ya Ghana, Black Stars, Raphael Dwamena amefariki dunia baada ya kuanguka uwanjani wakati wa mechi kati ya timu yake ya Egnatia Rrogozhine ya nchini Albania dhidi ya Partizani.
Mtandao wa soka wa Citi Sport umeripoti kuwa habari za kifo chake zimekuja baada ya mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 28 kupata mshtuko wa moyo dakika ya 23 ya mchezo na kusababisha kusimamishwa kwa mchezo huo.
Dwamena aligundulika kuwa na tatizo la moyo mwaka 2017 ambapo alifanyiwa upasuaji na kuwekewa kifaa cha kurekebisha mapigo ya moyo mwaka 2020.
Licha ya hatua hiyo ya matibabu, Dwamena alipata tena shida mwezi Oktoba 2021 alipoanguka uwanjani katika mchezo kati ya Blau-Weiss na Harterg katika Ligi ya Austria.