MBABE wa Yanga anayekipiga ndani ya kikosi cha Azam FC, Suleiman Abdallah, (Sopu) mambo kwake ni magumu ndani ya msimu mpya wa 2023/24 kwa kukosa zali la kucheka na nyavu kama ambavyo alianza msimu uliopita.
Mechi nne kapata zali la kuanza kikosi cha kwanza ndani ya Azam FC ambazo ni sawa na dakika 360 chini ya Kocha Mkuu Yusuph Dabo.
Timu hiyo ikwa imekomba pointi 19 na kufunga jumla ya mabao 19 hajatupia bao wala kutengeneza pasi ya bao ndani ya ligi msimu wa 2023/24.
Ikumbukwe kwamba kwa msimu wa 2022/23 nyota huyo alipopata zali la kucheza mechi 12 alitupia jumla ya mabao sita na pasi mbili za mabao.Kwenye mechi za mwanzo aliwaka na alianza kutoa pasi ya bao dhidi ya Yanga.
Mchezo huo uliochezwa Uwanja wa Mkapa, Septemba sita alitoa pasi moja ya bao dakika ya 65. Walipokutana kwenye mchezo wa mzunguko wa pili alifunga mabao mawili ilikuwa dakika ya 24 na 47 alimtungua Djigui Diarra.
Ikumbukwe kwamba alipokuwa ndani ya Coastal Union kwenye mchezo wa fainali ya Kombe la Shirikisho aliandika rekodi ya kufunga hat trick kwenye fainali na langoni alikuwa Diarra.
Ngoma ni nzito kwake msimu huu akiwa bado anajitafuta kurejea kwenye makali yake kwenye mechi za ushindani.