MASTAA sita kutoka Simba na Yanga nyota zao zimeonekana kuwaka kutokana na kuwa na zali katika kuhusika kwenye ushindi wa timu zao ndani ya dakika 90.
Mechi mbili tofauti za watani wa jadi walizotumia Uwanja wa Mkapa walikomba pointi tatu wote kwa nyakati zao. Ni Yanga 2-0 Singida Fountain Gate ngoma ilipigwa Oktoba 27, Simba 2-1 Ihefu hii ilipigwa Oktoba 28.
Kwenye mechi mbili jumla yalikusanywa mabao matano ambapo ni ukuta wa Simba ulikubali kutunguliwa kwenye mchezo huo walipokuwa nyumbani na langoni alianza Ally Salim.
Ni Moses Phiri wa Simba mwamba alitupia bao la ushindi kwenye mchezo dhidi ya Ihefu alipotumia pasi ya Luis Miquissone huku kila mmoja akifikisha namba tatu, Luis ni pasi za mwisho huku Phiri ikiwa ni idadi ya mabao aliyofunga kwenye ligi.
Mwingine ni Jean Baleke mshambuliaji wa Simba nyota yake iliwaka alipofunga bao la ufunguzi dakika ya 13 akiwa nje ya 18 baada ya beki wa Ihefu kujichanganya kwenye harakati za kutoa pasi.
Kwa upande wa Yanga ni Maxi Nzengeli huyu alitupia mabao mawili kwenye mchezo dhidi ya Singida Fountain Gate ilikuwa dakika ya 30 kwa pasi ya Yao Attohoula na Pacome Zouzoua aliyetoa pasi ya bao dakika ya 38.
Kivumbi kinatarajiwa kupigwa Uwanja wa Mkapa kwa watani wa jadi Novemba 5 kati ya Simba na Yanga.