MTAMBO wa mabao ndani ya kikosi cha Yanga, Maxi Nzengeli amesema kuwa wapo tayari kuelekea mchezo wao wa Karikoo Dabi dhidi ya Simba huku akiwaomba mashabiki wajitokeze kuona burudani.
Ndani ya kikosi cha Yanga Nzengeli ni chaguo la kwanza la Kocha Mkuu Miguel Gamondi akiwa kakomba dakika 489. Katupia mabao matano na pasi moja ya bao akihusika kwenye mabao saba kama namba ya jezi yake kati ya 20 yaliyofungwa na timu hiyo.
Mchezo uliopita dhidi ya Singida Fountain Gate walipokomba pointi tatu kwa ushindi wa mabao 2-0 ni yeye alitupia mabao yote kambani akimtungua Benedict Haule.
Nzengeli amesema: “Kikubwa ambacho tunafurahi ni kuona tunapata matokeo mazuri kwenye mechi ambazo tunacheza. Kuelekea mchezo wetu ujao tutafanya maandalizi mazuri na tunawaomba mashabiki wajitokeze kwa wingi.
“Ambacho ninaweza kusema ni kwamba kazi bado ipo na ushindani ni mkubwa. Mashabiki wamekuwa wakituongezea nguvu kwenye mechi ambazo tunacheza hivyo tunaamini tutaendelea kuwa wenye mwendelezo huu kila wakati,”.
Ni Novemba 5 watani wa jadi wanatarajiwa kumenyana kwenye mchezo wa Kariakoo Dabi, Uwanja wa Mkapa.