NI umakini kwenye safu ya kiungo, ulinzi na mlinda mlango wa Simba hawa ni tatizo ndani ya mechi tano mfululizo ambapo iliruhusu jumla ya mabao sita huku ile ya ushambuliaji ikitupia mabao 9.
Ndani ya dakika 450 ukuta wa Simba unatunguliwa bao moja kila baada ya dakika 75 huku safu ya ushambuliaji ikiwa na hatari kila baada ya dakika 50.
Mara ya mwisho Simba kupata clean sheet ilikuwa Septemba 21,2023 ubao wa Uwanja wa Uhuru ulisoma Simba 3-0 Coastal Union ilikuwa mchezo wa ligi.
Ngoma ilikuwa nzito Oktoba Mosi Simba 1-1 Power Dynamos, Uwanja wa Azam Complex. Katika mchezo huu wa Ligi ya Mabingwa Afrika, safu ya ulinzi ikiongozwa na Che Malone ilishindwa kufanya maamuzi ya haraka kupora mpira, mpigaji Andy Boyel alimtungua Ayoub Lakred dakika ya 15 akiwa nje ya 18.
Oktoba 5,2023 ubao wa Uwanja wa Sokoine ulisoma Tanzania Prisons 1-3 Simba. Katika harakati za kuokoa mpira, Che Malone alimchezea faulo nyota wa Tanzania Prisons. Pigo la faulo lilikuwa kwa Edwin Balua aliyemtungua Ally Salim akiwa nje ya 18 dakika ya 11.
Oktoba 8, Singida Fountain Gate 1-2 Simba, Uwanja wa Liti. Katika mchezo huu kipa Salim kwenye harakati za kuokoa hatari aliutema mpira ndani ya 18. Deus Kaseke hakuwa na ajizi aliujaza kimiani dakika ya 52.
Oktoba 20, Simba 2-2 Al Ahly mchezo wa robo fainali African Football League, Uwanja wa Mkapa. Bao la kwanza dakika ya 45 wakati Simba wakiwa kwenye umiliki eneo la kiungo walipoteza mpira uliokutana na nyota wa Al Ahly. Pasi ilipokutana na Red Slim alimtungua Salim.
Bao la pili lilifungwa kutokana na pigo la faulo iliyopigwa na nyota wa Al Ahly, ilipowapita mabeki wa Simba kipa Salim alitema mpira ndani ya 18 katika harakati za kuokoa ukakutana na mtupiaji Mahamoud Kahraba dakika ya 62.
Oktoba 24, Al Ahly 1-1 Simba, robo fainali ya pili AFL, Uwanja wa Taifa wa Cairo, Simba wakiwa wametoka kufunga bao kupitia kwa Sadio Kanoute, dakika ya 69, furaha yao ilidumu kwa dakika saba tu.
Kahraba alimtumgua Salim dakika ya 76 kwa kutumia makosa ya mabeki wa kati ambao walikuwa wanaamini yupo kwenye mtego wa kuotea.