SIO kila vita ni yakushinda unaambiwa hivyo lakini kuna wakali wa kazi wanaoonyesha utofauti kwenye kufanya kile ndani ya uwanjani.
Katika kikosi cha Simba kuna jamaa anaitwa Fabrice Ngoma ana balaa akiwa uwanjani kwenye pasi fupi na defu ambazo ni elekezi pamoja na uwezo wa mipira ile ya juu.
Nyota huyo iwe nyumbani ama ugenini anakiwasha kwa kuonyesha uwezo wake wa pasi ndefu na fupi. Alianza ugenini dhidi ya Mtibwa Sugar 2-4 Simba, Uwanja wa Manungu alikomba dakika 90.
Walipoibuka Mbeya, mchezo dhidi ya Tanzania Prisons 1-2 Simba, Uwanja wa Sokoine alikomba dakika 90 na kete ya tatu ugenini ilikuwa Singida Fountain Gate 1-2 Simba, Uwanja wa Liti alikomba dakika 90.
Kwenye mechi tatu za ugenini Ngoma kasepa na dakika 270 na msako wa pointi tisa zote zilikuwa halali yao mwisho wa mchezo.
Nyumbani anakiwasha
Mechi mbili za ligi kapata nafasi ya kucheza ilikuwa Simba 2-0 Dodoma, Jiji, Uwanja wa Uhuru alikomba dakika 45 na Simba 3-0 Coastal Union, Uwanja wa Uhuru dakika 90.
Nyumbani kakiwasha kwenye dakika 135 ukichanganya na zile 270 ngoma inakuwa imepigwa dakika 405 uwanjani.
Bao lake
Ni bao moja kwenye ligi mwamba kafunga ilikuwa kwenye mchezo wa ligi dhidi ya Mtibwa Sugar, Uwanja wa Manungu.
Huu ulikuwa ni mchezo wa ufunguzi kwa Simba inayonolewa na Kocha Mkuu, Roberto Oliveira kwenye ligi wakiwa ugenini.
Alipachika bao hilo dakika ya 44 kwa pigo la kichwa akiwa ndani ya 18 Agosti 17,2023 na Simba walikomba mazima pointi tatu.
Pasi ndefu na fupi zipo
Ngoma ana uwezo wa kupiga pasi ndefu na fupi namna anavypenda. Katika mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar alipiga pasi ndefu dakika ya 17.Mchezo dhidi ya Coastal Union alipiga pasi ndefu dakika ya 15, 26 pasi fupi alipiga dakika ya 26, 30 na alicheza faulo dakika ya 42.
Mchezo dhidi ya Tanzania Prisons alipiga pasi ndefu dakika ya 20, 21, 30, pasi fupi alipiga dakika ya tano.
Pointi 15
Ikiwa ni msimu wake wa kwanza ndani ya kikosi cha Simba ni shuhuda wakivuna pointi 15 kwenye mechi tano za ligi ambazo wamecheza.
Katika dakika 450 ambazo walishuka uwanjani kakosekana dakika 45 pekee nyingine zote kazikomba mazima.
Imeandikwa na Lunyamadzo Mlyuka, (Dizo Click) na imetoka gazeti la Championi Jumatatu.