KITAUMANA Oktoba 23 Uwanja wa Mkapa kwa wababe wawili kusaka pointi tatu muhimu ndani ya dakika 90. Yanga dhidi ya Azam FC watakuwa kazini kwenye mchezo wa Mzizima Dabi.
Yanga chini ya Kocha Mkuu, Miguel Gamondi inapambana kuendeleza rekodi nzuri ya kupata ushindi dhidi ya Azam FC wa mabao 2-0 walipokutana kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii, Tanga, Uwanja wa Mkwakwani.
Azam FC chini ya Kocha Mkuu, Yusuph Dabo inapambana kulipa kisasi cha kutunguliwa kwenye mchezo huo jambo linaloongeza ushindani mkubwa.
Tayari Gamondi yupo zake chimbo Avic Town akiwapa mbinu wachezaji wake ikiwa ni pamoja na Salim Aboubhakari, Hafiz Konkoni, Dennis Nkane, Skudu Makudubela na Jonas Mkude. Upande wa Azam FC wao kambi yao ipo Azam Complex wakiwa na nyota wao Feisal Salum, Prince Dube, James Akamiko, Ayoub Lyanga.
Gamondi ameweka wazi kuwa maandalizi kuelekea mchezo ujao wa ligi yanaanza baada ya kumaliza mchezo mwingine.
“Mechi zina ushindani mkubwa na wachezaji wanajitahidi kutimiza majukumu yao hilo ni kubwa hivyo kuelekea mechi zinazofuata tutazidi kufanyia kazi makosa yaliyopita kwenye mechi zetu,”.
Dabo amesema kuwa: “Kila mchezo una ugumu wake na hilo tunalitambua. Umakini kwa wachezaji ni muhimu na kupambana katika kutafuta matokeo ndani ya uwanja,”.
Timu zote mbili zilitoka kuvuna pointi tatu ugenini, ubao wa Kirumba ulisoma Geita Gold 0-3 Yanga na ubao wa Uwanja wa Mkwakwani ulisoma Coastal Union 0-1 Azam FC.