YANGA YAIPIGIA HESABU HIZI AZAM FC

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Bara, Yanga hesabu kubwa kwa sasa ni kuelekea mchezo wao wa ligi dhidi ya Azam FC unaotarajiwa kuchezwa Oktoba 23, Uwanja wa Azam Complex.

Chini ya Kocha Mkuu, Miguel Gamondi timu hiyo ilitoka kukomba pointi tatu dhidi ya Geita Gold kwa kushuhudia ubao wa Uwanja wa CCM Kirumba ukisoma Geita Gold 0-3 Yanga.

Itakutana na iwapinzan wao Azam FC waliotoka kukomba pointi tatu ubao wa Uwanja wa Mkwakwani, uliposoma Coastal Union 0-1 Azam FC na bao likijazwa kimiani na Feisal Salum anayefikisha mabao manne kwenye ligi.

 Gamondi amesema kuwa kila baada ya mchezo mmoja kuisha yanafuata maandalizi kwa mchezo unaofuata.

“Kila baada ya kukamilisha kazi kwenye mchezo wetu mmoja kinachofuata ni maandalizi ya mchezo wetu ujao. Kwenye ligi tunapambana kuona tunapata pointi tatu muhimu kwa wapinzani wetu ambao tunaamini nao wapo imara.

“Muhimu ni utayari na umakini kwa wachezaji kwenye kutumia nafasi ambazo tunazipata. Mbali na kuzipata ni muhimu kuongeza ulinzi kwani ili ushinde ni lazima usiruhusu kufungwa,” alisema Gamondi.

Miongoni mwa wachezaji wa Yanga ambao wameanza mazoezi kambini Avic Town Kigamboni ni pamoja na Skudu Makudubela, Jonas Mkude, Dennis Nkane, Pacome Zouzoah.