HIZI HAPA TIMU ZENYE WASTANI MZURI WA KUFUNGA BONGO

BADO haijafahamika nani atasepa na taji la ligi kutokana na mwanzo kuwa mgumu, ushindani ukipamba moto kila idara kuanzia ile ya ushambuliaji mpaka ulinzi.

Ikiwa ni mwanzo wa ligi kuna timu ambazo zina kasi kwenye utupiaji wa mabao zikiwa na wastani unaovutia kila zinaposhuka uwanjani. Nyingine bado zinajitafuta kufikia ile kasi waipendayo.

Hapa tunakuletea timu saba ambazo angalau zina wastani mzuri wa kufunga kwenye mechi za ligi namna hii:-

Yanga-15

Chini ya Kocha Mkuu, Miguel Gamondi hii ni namba moja kwa timu zenye wastani mzuri wa kucheka na nyavu. Baada ya mechi tano ambazo ni dakika 450 safu ya ushambuliaji imetupia mabao 15.

Kinara mwenye mabao mengi kwa mchezaji mmoja hakuna isipokuwa watatu wamegongana kwenye kutupia mabao matatumatatu. Aziz KI, Maxi Nzengeli na Pacome Zouozua hawa wote wanalijua lango lilipo.

Ni wastani wa kufunga bao moja kila baada ya dakika 30. Mbali na kuwa imara kwenye kucheka na nyavu ukuta wa Yanga ulitunguliwa mabao mawili kwenye mechi zote ilizoshuka uwanjani.

Simba -14

Ni mbinu za Roberto Oliveira zilitumika kwenye mechi tano kusaka ushindi. Safu ya ushambuliaji ilitupia mabao 14 ikiwa ni namba mbili kwa timu zilizofunga mabao mengi kwenye ligi.

Ina wastani wa kufunga bao moja kila baada ya dakika 32. Kinara wa kutupia mabao kwenye kikosi hicho ni mshambuliaji Jean Baleke ambaye katupia mabao matano.

Azam FC – 10

Matajiri wa Dar, ni timu kubwa inayomiliki Uwanja wa Azam Complex. Ni mabao 10 safu ya ushambuliaji ilitupia ndani ya dakika 450. Ni namba tatu kwenye ukali wa kucheka na nyavu.

Namba moja anaitwa Feisal Salum yeye ni kinara ndani ya timu hiyo akiwa katupia mabao manne. Ina wastani wa kufunga bao moja kila baada ya dakika 45.

Yusuph Dabo raia wa Senegel anawanoa vijana hao ambao mchezo ujao kwenye ligi itakuwa dhidi ya Yanga.

KMC, Mtibwa Sugar na Tanzania Prisons -6

Timu tatu zina wastani wa kufunga bao moja kila baada ya dakika 75. Sio kasi bora kwa timu hizi hivyo zina kibarua cha kufanyia kazi safu zao za ushambuliaji kuwa imara kwenye mechi zijazo za ligi.

Mbali na maboresho upande wa ushambuliaji rekodi zinaonyesha kuwa timu hizo kuna shida kwenye ukuta kwa kuruhusu mabao mengi kwenye mechi walizocheza.

KMC ilifungua pazia kwa kufungwa mabao mengi na Yanga ilikuwa mabao matano Uwanja wa Azam Complex. Kwenye mechi tano ni mabao 8 timu hiyo ilitunguliwa.

Mtibwa Sugar kwenye dakika 450 ilitunguliwa mabao 10 wastani wa kufungwa bao moja kila baada ya dakika 45 huku Prisons ikitunguliwa mabao 11 wastani wa kuokota nyavuni bao moja kila baada ya dakika 40.

Tabora United-5

Ni msimu wake mpya ndani ya ligi ikiwa na wastani wa kufunga bao moja kila baada ya dakika 90. Angalau inaingia kwenye orodha ya timu saba ambazo zina uchu wa kufunga mabao kwenye mechi wanazocheza.

Ukuta wake ni mabao sita ulitunguliwa hivyo benchi la ufundi bado lina kazi kuimarisha pande zote mbili, kuanzia ile ya ushambuliaji na ile ya ulinzi ili kufikia malengo.

Imeandikwa na Lunyamadzo Mlyuka, (Dizo Click) na kutoka gazeti la Spoti Xtra.