MATOKEO ya mchezo wa mpira wa miguu yanashangaza kutokana na kila timu kutumia makosa ya wapinzani. Ili kushinda ni muhimu kutumia kila nafasi ambayo inapatikana ndani ya dakika 90.
Kwa sasa Simba wawakilishi wa Tanzania kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika wana kazi ya kusaka ushindi Oktoba 20 kwenye mchezo dhidi ya Al Ahly.
Mchezo huu wa Al Ahly timu yenye rekodi bora Afrika hautakuwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika. Ni mchezo wa African Football League ambao unatarajiwa kuchezwa Uwanja wa Mkapa.
Kikubwa kuelekea kwenye mchezo huu ni muhimu kwa wachezaji kutambua kwamba hautakuwa mwepesi kama ambavyo wanafikiria.
Mbele ya wageni wakubwa wa soka duniani hakuna timu itakayokubali kupoteza ipo hivyo. Ni muda wa kufanya maandalizi mazuri kwa ajili ya kupata matokeo mazuri.
Mashabiki mtakaojitokeza msibebe matokeo mfukoni kwa kuwa hakuna anayetambua nini kitatokea baada ya dakika 90.
Muhimu ni kila mmoja kuwa na imani kuwa mchezo ni mchezo ambao hautabiriki na kila timu inahitaji ushindi ndani ya uwanja. Kila kitu kinawezekana kwenye soka ikiwa kutakuwa na mipango makini.
Muda ni sasa wa kuacha kasumba ya kubeba matokeo uwanjani na badala yake kuwa mashuhuda mpaka dakika 90 zitakapokamilika.
Wachezaji fanyeni kweli kutafuta ushindi kuwapa furaha mashabiki kwa kuwa hapo ndipo furaha ilipojicha kwenye ushindi.