KUFUZU AFCON HAITOSHI, LAZIMA TUJIONDOE NAFASI YA KIBONDE

TAYARI kikosi cha timu yetu ya taifa, Taifa Stars kimefanikiwa kufuzu kucheza michuano mikubwa zaidi Africa maarufu kama Afcon kwa 2023.

Mambo yatakuwa nchini Ivory Coast na katika kundi tulilopangwa licha ya kwamba inaonekana si uzalendo kusema lakini lazima isemwe kuwa timu inayopewa nafasi ya mwisho kabisa katika kundi hilo ni Tanzania.

Yes, sisi ndio tunapewa nafasi ya mwisho kwa kuwa kuna Morocco lakini majirani zetu wawili kwa maana ya DR Congo na Zambia. Wao katika michuano hii ni mara kwa mara.

Ndio maana Tanzania ilikuwa katika port four kutokana na uhalisia. Sasa hapo ndipo kunatakiwa tukubaliane napo kuwa lazima tuende katika michuano hiyo tukiwa tayari tunajua kuna kazi ya ziada ya kufanya.

Michuano ya mwisho ya Afcon ambayo tulishiriki, tuliishia katika nafasi ya mwisho ya kundi licha ya kwamba tulikuwa na majirani zetu Kenya ambao hata nao walitufunga.

Kama michuano hii nayo tutaishia katika nafasi ya mwisho ya kundi, lazima tujue tutaendelea kubaki katika port four ambayo si vibaya kusema ni vibonde wa kundi.

Tunakwenda Ivory Coast si kwa ajili ya kuendelea kushiriki, lengo ni kupambana na kubadilisha historia ya Tanzania katika michuano hii mikubwa.

Nchi yetu tokea 2019 hadi 2023 imefanikiwa kucheza michuano hiyo mara mbili. Hili si jambo dogo kwetu na haikuwahi kuyokea hata kidogo huko nyuma.

Sasa kama tumeweza hili, lazima tubadilishe tena suala la sisi kuona kufuzu peke yake kunatosha kwa maana ya kwenda kushiriki na kurudi nyumbani na ikawa inatosha kabisa.

Lazima tuende na mawazo tofauti, kwamba tunakwenda Ivory Coast kushindana na malengo yawe angalau kufika robo fainali na ikishindikana kabisa basi kuingia hatua ya mtoano ambayo itakuwa ni mara ya kwanza.

Kizazi hiki ndicho kimeandika hiyo rekodi ya kucheza Afcon mara mbili mfululizo ndani ya miaka mitano tu. Kama unakumbuka kabla yam waka 2019, Tanzania ilicheza Afcon kwa mara ya mwisho mwaka 1980.

Tofauti hii sasa inapaswa kuingia vichwani mwetu na ianzie kwa wachezaji kuwa inawezekana tofauti na inavyofikiriwa kwa kuwa pia ilifikiriwa ni vigumu kwa Tanzania kuzufu Afcon katika kundi ambalo lilikuwa na timu za Algeria, Niger na Uganda.

Kwenye kundi hilo, pia sisi ndio tulikuwa vibonde wa kundi, lakini tukafanikiwa kutoka kibabe kwa kupata pointi moja ya mwisho ugenini dhidi ya Algeria, timu ambayo ilitufunga nyumbani Tanzania lakini imekuwa ikitufunga kila tunapokanyaga ardhi ya kwao.

Kuibadilisha Tanzania ikajikomboa na kutokuwa mwisho katika makundi kila yanapopangwa inawezekana kabisa. Hili halitakuwa jambo geni kwa wachezaji wa Kitanzania kwa kuwa kuna mfano tena uko karibu kabisa.

Miaka 10 au 15 tu iliyopita, katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika, sasa Ligi ya Mabingwa, Kombe la Shirikisho, timu zetu zilionekana hazina nafasi kabisa na hakuna aliziwazia hata kufikia hatua ya mtoano.

Kila kundi la klabu bingwa lilipopangwa, timu zetu zilikuwa chungu cha nne. Lakini taratibu Simba wakaanza kuleta mabadiliko na mapinduzi ambayo yamekuwa hamu ya timu nyingi za Tanzania kutaka kutenda na imewezekana.

Licha ya kwamba katika michuano kama minne Simba imeishia robo fainali, lakini angalia kuna wakati Simba iliongoza kundi ambalo ndani yake kulikuwa na mabingwa mara nyingi zaidi Afrika Al Ahly ikiwa ni pamoja na kuwafunga jijini Dar es Salaam.

Mwendo wa Simba ukabadilisha mambo Simba yenyewe, klabu nyingine, mfano uliona Namungo ikienda makundi Kombe la Shirikisho, Yanga msimu uliopita ikafika fainali michuano hiyo.

Msimu huu kuna hatua kubwa imepigwa, Simba wameingia hatua ya makundi, Yanga pia wamefanya hivyo na tayari hii ni rekodi mpya kwetu, haijawahi kutokea kabla maana wababe hawa wawili wameingia hatua hiyo kwa pamoja.

Wakati wa upangaji wa ratiba, Simba walikuwa chungu cha pili, Yanga walikuwa chungu cha tatu na katika timu hizi mbili za Tanzania hakuna aliyekuwa chungu cha nne kwa maana ya kibonde.

Klabu zetu zimeonyesha mfano kuwa uwezekano wa kukomboka upo tena ni mkubwa kwa kuwa wachezaji Watanzania pia wapo katika timu zetu hizo mbili na wanategemewa.

Kama wawezeka kushiriki katika kuzikomboa klabu, sasa wnaashindwaje kulihamishia hilo katika timu yetu ya taifa na mwisho tukavuka hatua ya makundi na kuingia mtoano ili kuonyesha pia inawezekana kwa vitendo kwa kuwa kweli inawezekana!

Muda ndio huu na wakati umewadia. Tulifanye hilo ili kuendelea kuleta mabadiliko katika mpira wetu. Hakuna anayeweza kufanya hayo mabadiliko, isipokuwa Watanzania wenyewe.