MAKUBALIANO ya pande zote mbili kati ya uongozi wa Ihefu na Zuberi Katwila ambaye alikuwa kocha mkuu wa timu hiyo yaliamua mwisho wa Katwila kuwa ndani ya kikosi hicho.
Kwa mujibu wa taarifa iliyochapishwa na klabu hiyo kwenye ukurasa wake wa Instagram, Oktoba 14,2023 Ihefu SC haitakuwa na Katwila kwenye benchi la ufundi baada ya kumpa mkono wa asante.
Timu hiyo imeweka wazi kuwa inamshukuru kwa wakati wote aliohudumu katika viunga vya Highland Estates tangu ajiunge mwaka 2020.
Taarifa zinaeleza kuwa baada ya mchezo dhidi ya KMC wachezaji na benchi la ufundi walikuwa kwenye mapumziko na siku ya kurejea kambini naye alirejea kuendelea na majukumu yake.
“Timu ilikuwa imepewa mapumziko na kocha pia hakuwa kambini. Siku ya kurejea kambini ilipofika bosi alimuita na kuongea naye wakafikia makubaliano ya kuondoka.
“Hakuna makosa ambayo amefanya basi tu imeamuliwa kuwa hivyo sababu ni kutaka kupata benchi jipya kwenye timu,” ilieleza taarifa hiyo.
Oktoba 4, Katwilaaliongoza benchi laufundi kuandika rekodi ya kuwa timu ya kwanza kuwafunga mabingwa watetezi ambao ni Yanga.
Baada ya dakika 90 ubao wa Uwanja wa Highland Estate ulisoma Ihefu 2-1 Yanga. Mabao ya Lenny Kissu na Ilanfya yaliipa pointi tatu Ihefu na lile la Yanga lilifungwa na Pacome.
Mchezo wa mwisho kukaa benchi ilikuwa ni Oktoba 7 ubao wa Uwanja wa Uhuru ulisoma KMC1-0 Ihefu ukiwa ni mchezo alioyeyusha pointi tatu ugenini.