UNAWEZA ukaona kama mzaha hivi lakini ubora wa Ligi kuu Bara unajidhihirisha, mapema sana katika raundi ya tano tumeanza kuona mengi.
Ihefu akiwa mgeni wa KMC ya Kinondoni. Mechi ikapigwa kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam. Ihefu walipoteza mchezo huo kwa kufungwa bao 1-0.
Ihefu walikuwa wanaingia uwanjani baada ya kuwa wa kwanza msimu huu kama ilivyokuwa msimu uliopita, kumtwanga bingwa mtetezi na kumuandikia kipigo cha kwanza. Waliishinda Yanga kwa mabao 2-1.
Vijana hao kutoka Mbarali walikuwa walikutana na KMC ambayo katika mechi ya ufunguzi wa Ligi Kuu Bara, walikutana na kipigo cha mabao 5-0 kutoka kwa Yanga.
Hapa ilikuwa ni myonge wa Yanga aliyekuwa nyumbani dhidi ya wababe wa Yanga waliokuwa ugenini. Mechi ungeipigia hesabu za kawaida, ungesema KMC walipaswa kuadhibiwa na Ihefu ambao ni wababe wa wababe zao, mwisho Ihefu kalala kwa bao 1-0.
Maana yake, utasema hivi, Yanga ni mbabe wa KMC, halafu Ihefu ni mbabe wa Yanga lakini KMC naye ni mbabe wa Ihefu. Kila mmoja na mnyonge wake.
Hii inaonyesha kuwa hakuna mwenye uhakika wa kushinda kila anapokutana na mwingine, hii inaonyesha kuwa ligi ni ngumu kwa kuwa haina mwenyewe ambaye anaweza kujiona hakamatiki.
Yanga baada ya kipigo cha ugenini, wamerejea na kuitwanga Geita Gold kwa mabao 3-0 ikiwa ‘nyumbani’ jijini Mwanza. Siku ambayo Ihefu walioshinda nyumbani dhidi ya Yanga wakikutana na kipigo.
Mabingwa watetezi Yanga wamerejea tena kwa kasi, wakiwa na funzo kubwa au gumu kwamba ligi si nyepesi na haitaki hadithi tena.
Ligi imesimama kwa maana iko imara na kila upande wa kila timu unataka kushinda au kufanya bora zaidi. Hivyo hakuna anayetabirika.
Ligi ngumu kubashiri maana yake ubora umepanda na hii ndio maana unaona, hata baada ya kupoteza, kasi waliyorejea nayo Yanga inaonyesha kuwa bado ni timu bora ambayo haijayumbishwa na kipigo cha Ihefu.
Ndani ya Yanga, kuna wachezaji wakomavu ambao wanatambua nini maana ya kipigo na wanataka kufanya jambo zuri au bora hata wanapokuwa katika wakati mgumu.
Ushindani wa namna hii unazidi kuimarisha kiwango cha ushindani baina ya timu na timu na kinaondoa unyonge kati ya timu kubwa na ndogo.
Ushindani sahihi ni ule ambao unaifanya kila timu kulazimika kujitafakari upya kila baada ya mchezo na kila inapoingia uwanjani hakuna timu inakuwa na uhakika wa kupata ushindi kwa kuwa matokeo hupatikana baada ya dakika 90.
Simba na Yanga licha ya ukubwa wao, sasa ni moja ya timu gumzo katika bara la Afrika na moja ya timu 16 zilizoingia hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Bado unaziona zinavyolazimika kupambana hasa ili kuibuka na ushindi au kupata pointi tatu katika Ligi Kuu Bara.
Ligi inazidi kuimarika na hii inaongeza ushindani na kwa kiasi kikubwa inasaidia kuimarika kwa timu zote na kufanya kiwango cha ushindani kizidi kupanda.
Kila kiwango cha ushindani kinavyopanda, maana yake ubora unapanda pia na kuwaongezea wachezaji na vikosi vyao uimara na mwisho, ligi inazidi kuimarika.
Kikubwa kwa sasa ni hali iliyopo ya ushindani ambayo imeanza mwanzoni kabisa mwa ligi, iendelee. Isifikie sehemu zibaki Simba, Yanga, Azam na Singida Fountain Gate.