KAZI KIMATAIFA NI KUBWA MIPANGO MUHIMU

BAADA ya makundi kupangwa kwa sasa ni muda wa kuanza kufanya maandalizi kwa ajili ya kupata matokeo chanya kwenye mechi za ushindani.

Katika Ligi ya Mabingwa Afrika hakuna kubeba matokeo mfukoni wala kuamini kwamba uzoefu utawabeba katika kupata ushindi hilo halipo.

Kuanza kubeba matokeo wakati huu na kujipeleka hatua ya robo fainali anguko linakuja. Hakuna timu iliyopita kwa bahati mbaya kila timu ilikuwa na mipango.

Ile mipango iliyopangwa kwenye hatua za mwanzo inapaswa kuwa endelevu. Muda uliopo kwa sasa ni kuwekeza nguvu kubwa kwenye maandalizi.

Tambo za Yanga na Simba hazikosekani lakini ukweli utabaki palepale kwamba sio Simba wala Yanga mwenye uhakika wa kutinga hatua ya robo fainali.

Ili utinge robo fainali ni lazima upate matokeo na hesabu huku ni pointi. Kupata pointi sio jambo jepesi maandalizi ni sasa kuelekea kwenye mashindano hayo makubwa.

Kelele na porojo hazina nguvu ya kuleta matokeo na timu kutinga hatua ya makundi. Kukwama kupanga mipango mizuri sasa ni muda wa kutengeneza anguko kesho.

Wakati ni sasa kuendelea kufanya maandalizi mazuri kwenye mechi za kimataifa. Hakuna muda wa kupoteza na kuanza kutamba kwamba timu itapenya kwa kuwa ina wapinzani dhaifu.

Kila mmoja anatafuta pa kutokea hata wale ambao mnawaona ni wepesi na wao pia wanawaona sehemu watakayokomba pointi ni kwenu.