KUNA kila sababu ya kusema Serikali ya Jamhuri ya Tanzania chini ya Dk Samia Suluhu Hassan inajitahidi kuonyesha inafanya jambo katika michezo nchini.
Inawezekana kwa awamu kadhaa zilizopita, Serikali imekuwa ikishiriki katika michezo katika nyanja mbalimbali.
Kipindi hiki kumekuwa na mabadiliko zaidi na mengi yanahusisha hamasa na kidogo usaidizi katika gharama ya timu zetu za taifa na hata klabu zinazoshiriki michuano ya kimataifa.
Tumeona namna kumekuwa na chachu kupitia Goli la Mama, Dk Samia amekuwa akitoa fedha za hamasa kwa kila bao linalopatikana na alianzia katika Kombe la Shirikisho la Caf na Ligi ya Mabingwa Afrika.
Msimu uliopita Tanzania ikang’ara, timu mmoja ikaenda fainali ya Kombe la Shirikisho kwa maana ya Yanga na nyingine ambayo ni Simba ikaishia robo fainali katika Ligi ya Mabingwa Afrika.
Hamasa hiyo tumeona imeendelea hadi kwenye timu za taifa na hakika imekuwa sehemu ya chachu vijana kuendelea kupambana na kutaka kufanya vizuri.
Kwa sasa Tanzania imeendelea kuwa gumzo katika michuano kadha wa kadha ya mchezo wa soka barani Afrika.
Hivi karinbuni, Taifa Stars chini ya Kocha Adel Amrouche imeendelea kushaini na kuandika rekodi nyingine ya kuzufu kucheza Afcon kwa mara ya tatu.
Nakukumbusha, Mama Samia aliahidi wakifuzu, atawapa Sh milioni 500 au nusu bilioni. Hilo limefanikiwa na juzi, Waziri Mkuu, Majaliwa Kassim Majaliwa amewakabidhisha kiasi hicho cha fedha, maana yake ahadi imetolewa na imetekelezwa mara moja.
Ukisema katika kipindi hiki Serikali haishiriki katika michezo, utakosea na unaweza ukaona soka ndio ni kama inapendelewa lakini ukweli ni kwamba soka wanajitutumua na kujituma kwenda kwenye mafanikio na kuitangaza nchi yetu na jambo jema zaidi wakapewa ushirikiano zaidi.
Pamoja na yote hayo, bado mimi nilikuwa nina wazo kuwa Serikali ina uwezo ikiamua, uwezo kuchukua gharama za maandalizi ya timu zetu ili kuzifanya kuwa bora zaidi.
TFF pamoja na kufanya vizuri lakini imekuwa ikizidiwa na wingi wa mashindano ya timu zake. Mfano unaona kuna timu za vijana za wanawake na wanaume chini ya miaka 17 zina mashindano, kuna vijana chini ya miaka 20 pia katika mashindano ya kuwania kucheza Kombe la Dunia lakini Olimpiki pia.
Kuna mashindano kwa ajili ya timu ya wanawake ya wakubwa Twiga Stars, nao wanawania kucheza mashindano makubwa chini ya Fifa na Caf pia. Lakini kuna Taifa Stars ambayo inahitaji kambi kubwa na bora ambayo itaifanya kuwa bora zaidi na tayari kwa mashindano.
Kama Serikali itaendelea kuiachia TFF na kusubiri panapokuwa na hamasa ndio wajitokeze, inawezekana wakawa wanafanya jambo lakini lisiwe kubwa sana au lenye nguvu zaidi kama watakuwa wakishirikiana na TFF kuanzia mwanzo kabisa.
Inawezekana kama wataamua, sitaki kusema hivi lakini kama ni sehemu ya mfano naweza kukumbushia tu kuwa nchi kama Rwanda inawezaje kuzihudumia timu zake za taifa lakini hata klabu zinazoshiriki michuano ya kimataifa halafu nchi kama Tanzania ishindwe kufanya hivyo?
Ninaamini kabisa tunajiweza na tunaweza kufanya hivyo mara kumi ya Rwanda lakini ilikuwa ni suala la kusubiri njia yakupita na kufika kupita hadi tulipofikia.
Wanaousimamia mpira kwa maana ya TFF kwa kweli wameonyesha nia na uwezo wa kufikia malengo kwa kufanya vizuri.
Bila shaka, unayemsaidia naye anapaswa kuonyesha huo msaada alikuwa anauhitaji na akiupata ataonyesha mabadiliko n hatua na hili TFF wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa.
Sasa kama watasaidiwa zaidi na kupewa maandalizi ya kutosha ikiwemo kupunguziwa gharama kwa maana ya Serikali kuzishikilia, bila shaka kutakuwa na mafanikio makubwa zaidi.
Nashauri Serikali iliangalia hili na ninaamini kutakuwa na faida kubwa baadaye kwa maana ya kufungua zaidi wigo wa ajira zaidi lakini kuendelea kuliheshimisha na kulitangaza taifa letu zaidi.