KUVUNJIKA KWA KOLEO SI MWISHO WA UHUNZI

KWENYE anga la kimataifa tumeona namna ambavyo wawakilishi wa Tanzania walikuwa wakipambana kutafuta matokeo. Mwisho dakika 90 zimeamua nani atakuwa nani.

Kwa Yanga walikuwa na faida ya ushindi wa mabao mawili waliyopata ugenini dhidi ya Al Merrikh na Simba wao sare ya mabao 2-2 waliyopata ugenini.

Ni wazi kuwa wachezaji wa Yanga walijituma mechi zote mbili kuonyesha ushindani. Kusonga mbele bila kuruhusu mabao ya kufungwa hili wanahitaji pongezi.

Kikubwa ni namna wachezaji wanavyoshirikiana katika kutimiza majukumu yao. Jumla mabao 3-0 yanawapa nafasi ya kusonga mbele kimataifa.

Ukija kwa upande wa Simba bado wanajitafuta kwenye aina ya uchezaji wao.Kwa wakati huu kuna umuhimu wa benchi la ufundi kutafuta mbinu mpya ambazo zitakuwa na mabadiliko kwa wakati ujao.

Kusonga mbele kwa faida ya mabao ya ugenini hilo ni jambo moja lakini ni muhimu timu kucheza kwa kushirikiana na sio kutegeana kwenye majukumu.

Singida Fountain Gate walikuwa na nafasi pia ya kufuzu hatua ya makundi. Kupoteza kwa kufungwa mabao 4-1 dhidi ya Future kumewapoteza ramani wawakilishi katika anga la kimataifa.

Ni ngumu lakin ni mwanzo ambao unahitaji umakini kwa wakati ujao. Kupata nafasi nne kwenye anga la kimataifa na mwisho ikawa ni timu mbili kuna namna inapaswa kufanyika.

Kuvunjika kwa koleo sio mwisho wa uhunzi wanasema hivyo kazi inapaswa kufanyika kwa timu zote ambazo zipo ndani ya Bongo.