>

MKALI WA MABAO SIMBA AFUNGUKIA ISHU YAKE NA KOCHA

MSHAMBULIAJI wa Simba, Moses Phiri amevunja ukimya kwa kusema hana tatizo lolote na Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mbrazil, Robert Oliveira ‘Robertinho’ kutokana na kukosa nafasi ya kucheza muda mrefu.

Msimu wa 2022/23 Phiri alitupia kibindoni mabao 10 na alikuwa shuhuda mfungaji bora akitokea Yanga na mwingine Simba.

Ni Fiston Mayele wa Yanga na Saido Ntibanzokiza wa Simba hawa walitwaa tuzo ya ufungaji bora baada ya kutupia mabao 17 kila mmoja kwenye ligi.

Kwa sasa Mayele hayupo ndani ya Yanga akiwa kwenye changamoto mpya huku Ntibanzokiza bado yupo ndani ya kikosi cha Simba.

Phiri ‘General’ ametoa kauli hiyo kufuatia kuwepo kwa taarifa za kuhusishwa na kuomba uongozi wa timu hiyo umpe ruhusa ya kuweza kuondoka kufuatia madai ya kuwa haelewani kocha mkuu wa timu hiyo kitu ambacho kimesababisha akose nafasi ya kucheza ndani ya timu hiyo.

 Phiri amesema hakuna ukweli juu ya kutaka kuondoka ndani ya kikosi cha timu hiyo na kuweka wazi ataendelea kusalia ndani ya klabu hiyo huku akisisitiza kuwa hana matatizo na Robertinho licha ya yeye kukosa nafasi ya kucheza kwa muda mrefu ndani ya timu hiyo.

“Bado nipo sana Simba, nina mkataba nao hakuna ukweli kuwa nataka kuondoka hapa, nafuraha na timu yangu na nitaendelea kupigana klabu yangu kila mechi kuhakikisha wanapata kile wanachokitarajia.

“Nipo Simba na bado mimi ni mchezaji wao, sijawahi kuwa na mgogoro na kocha ila anashindwa kupata nafasi ya kucheza kwa sababu ya kutoka katika majeraha ambayo yaliniweka nje muda mrefu, napewa muda mdogo ili kuweza kurudi taratibu kuweza kupambana hakuna kitu kingine,” amesema Phiri.