SIMBA YAJA NA ONYO ZITO

LICHA ya kufanikiwa kuibuka na pointi sita
katika michezo yao miwili ya kwanza ya Ligi Kuu Bara, Kocha Mkuu wa Simba, Mbrazili, Roberto Oliviera ‘Robertinho’ amewaonya mastaa wa timu hiyo.

Miongoni mwa nyota hao ni Clatous Chama na Luis Miqquisone kuhakikisha hawabweteki bali
wanapambana kuhakikisha wanashinda kila
mchezo ulio mbele yao.

Ipo wazi kuwa Simba ilipishana na ubingwa wa ligi msimu wa 2022/23 uliokwenda kwa watani zao wa jadi Yanga.

Yanga wameanza kwa kasi msimu wa 2023/24 kwa kupata ushindi wa mabao 5-0 KMC kwenye mchezo wa ufunguzi uliochezwa Uwanja wa Azam Complex.

Robertinho ameyasema hayo mara baada ya
kuiongoza Simba kushinda michezo miwili ya
kwanza kwenye Ligi Kuu Bara dhidi ya Mtibwa
Sugar na Dodoma Jiji ambapo kutokana na
matokeo hayo Simba sasa wanaongoza
msimamo na pointi zao sita.

Akizungumzia maendeleo ya kikosi chake,
Robertinho alisema: “Kwa nafasi ya pekee nawapongeza wachezaji wangu kwa matokeo
mazuri ambayo tumefanikiwa kuyapata katika
michezo yetu miwili ya kwanza.

“Licha ya mafanikio hayo lakini nimezungumza
na wachezaji wangu kuwakumbusha kuwa bado kazi haijaisha na hatupaswi kubweteka, bali ni lazima tuhakikishe tunashinda kila mchezo ulio mbele yetu.

“Ni wazi kadiri siku zinavyozidi kwenda
wachezaji wanazidi kuzoeana na naamini kuwa
mbeleni tutapata nafasi ya kucheza soka bora
zaidi baada ya wachezaji wote kupata muda wa
kuelewana vizuri.”