>

GONJWA LINALOITESA SIMBA LAHAMIA YANGA

IPO wazi kuwa maumivu yanayowatesa mastaa wa Simba wakiongozwa na Clatous Chama na Saido Ntibanzokiza yanawaliza na mastaa wa Yanga kwenye anga la kitaifa na kimataifa.

Ni janga la kutumia mapigo huru ya kona kwenye mechi zao wanazocheza kuwa ni hasara kubwa kwa kuwa hakuna iliyowapa bao ama kusababisha bao wakiwa uwanjani.

Simba chini ya Kocha Mkuu, Roberto Oliveira reodi zinaonysha kuwa kwenye mchezo wa ligi dhidi ya Mtibwa Sugar ilipata kona zaidi ya 10 huku wapigaji wakiwa ni Chama, Ntibanzokiza na Mzamiru kona zao zote ziliokolewa na wapinzani.

Hata faulo ambazo zilipatikana kwenye mchezo huo uliochezwa Uwanja wa Manungu, Agosti 17 ubao uliposoma Mtibwa Sugar 2-4 Simba, Chama alipiga faulo zaidi ya nne huku Ntibanzokiza zaidi ya mbili zote hazikufua dafu.

Yanga yenye mtaalamu Aziz KI kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya ASAS Djibout rekodi zinaonyesha kuwa ilipata jumla ya kona 10 na katika hizo hakuna hata moja iliyoleta bao.

Kete ijayo kwa Yanga ni mchezo wa ligi dhidi ya KMC unaotarajiwa kuchezwa Uwanja wa Azam Complex, Agosti 23 ukiwa ni mchezo wa kwanza kwa Yanga msimu wa 2023/24.