BAADA ya kungoja kwa muda hatimaye kesho ukurasa mpya wa msimu wa 2023/24 unafunguliwa kwa mechi za moto mkali ambazo zitakuwa ni tatu kwa kuchezwa viwanja tofauti.
Ikumbumbukwe kwamba mabingwa watetezi wa taji la ligi ni Yanga ambao walikuwa na kibarua cha kutetea Ngao ya Jamii.
Yanga ni mashuhuda Agosti 13 Ngao ya Jamii ikielekea kwa watani zao wa jadi Simba.
Chini ya Kocha Mkuu, Miguel Gamondi wanarejea Dar kuanza maandalizi ya ligi na mchezo wa kwanza kwa Yanga itakuwa dhidi ya KMC, Uwanja wa Azam Complex.
Kila timu itakuwa na kazi ya kusaka pointi tatu katika dakika 90 za moto ambapo ni Ihefu itafungulia ikiwa nyumbani, Uwanja wa Highland Estate, Mbeya.
Chini ya Kocha Mkuu, Zuberi Katwila Ihefu itamenyana na Geita Gold inayonolewa na Kocha Mkuu, Hemed Morocco.
Ikumbukwe kwamba Ihefu imesajili nyota wapya ikiwa ni pamoja na kiungo Victor Ackpan kutoka Simba mshambuliaji Charles Ilanfya kutoka Mtibwa Sugar,kipa Haroun Mandanda aliyekuwa Mbeya City ikiwa ni baadhi ya nyota wapya katika kikosi hicho.
Dakika 90 nyingine za moto ni kwenye mchezo wa Namungo dhidi ya JKT Tanzania huu unatarajiwa kuchezwa Uwanja wa Majaliwa.
JKT Tanzania ambayo imepanda Ligi Kuu Bara msimu wa 2023/24 itakuwa ugenini ikikaribishwa na Namungo FC inayonolewa na Kocha Mkuu, Cedrick Kaze ambaye msimu wa 2022/23 alikuwa ndani ya kikosi cha Yanga.
Kete ya tatu inayotarajiwa kuonekana kesho ni Dodoma Jiji hawa watawakaribisha Coastal Union katika Uwanja wa Jamhuri, Dodoma.
Kivumbi cha Ligi Kuu Bara kinatarajiwa kuanza Agosti 15 ikiwa ni msimu mpya wa 2023/24.