HATIMAYE Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na Benki ya NBC wametangaza kufanya maboresho ya mkataba wao wa udhamini wa Ligi Kuu Bara, kutoka udhamini wa awali wa miaka mitatu hadi mitano kuanzia msimu wa mwaka 2023/24 hadi mwaka 2027/2028.
Ikumbukwe kuwa udhamini wa awali wa miaka mitatu ulikuwa wa thamani ya sh. Bilioni tisa ilikuwa kuanzia 2021/22 na ulitarajiwa kumalizika msimu ujao wa mwaka 2023/2024.
Hivyo sasa mktaba mpya utakuwa na thamani ya sh. Bilioni 32.6 ambao una kipengele cha udhamini wa michuano ya Championship na Ligi ya Vijana ya umri chini ya miaka 20 na zote zitapewa majina ya benki hiyo baada ya utaratibu kukamilika.
Akizungumza katika hafla ya kutiliana saini ya mkataba huo, Rais wa TFF, Wallace Karia, alisema udhamini huo mpya utaongeza thamani ya soka la Tanzania kuanzia Ligi Kuu hadi Ligi ya Vijana.
“Ushirikiano kati ya na NBC, utakwenda kuongeza thamani ya michuano ya Ligi Kuu Tanzania Bara, michuano ya Championship na Ligi ya Vijana chini ya umri wa miaka 20 ambayo kuanzia msimu ujao itachezwa kwa mechi za nyumbani na ugenini.
“Tunatarajia kuzipa ligi hizo majina mengine baada ya kumalizika kwa utaratibu kati yetu na wadhamini, tunawaomba wadhamini mbalimbali kujitokeza kuendelea kudhamini michuano mbalimbali.
Aliongeza kuwa katika mkataba huo, TFF haitaruhusu wanachama wake kutumia kwa manufaa yoyote washindani wa kibiashara wa mdhamini wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC, Theobald Sabi, alisema benki hiyo imeona manufaa ya kudhamini mpira wa Tanzania na ndiyo sababu ya kuingia mkataba huo mpya.
“Kupitia mpira katika udhamini wetu wa awali tumeona kupanda kwa thamani ya chapa yetu, tunajivua hilo na ndiyo maana tulianzisha mazungumzo ya kuongeza udhmaini wetu ambao utashuka mpaka katika ligi za vijana na ile ya Championship, tunashukuru sana na tunajivunia hilo
“Kwa kipindi chote tangu tuanze kudhamini michuano ya Ligi Kuu Tanzania Bara, tumeona mafanikio makubwa ikiwemo kupanda zaidi kwa thamani ya ligi yetu na kushika nafasi tano za juu ikiwemo kuvutia wachezaji kutoka nje ya nchi ambapo wamekuwa wakija kusajiliwa nchini,” alisema Sabi.