SASA ni rasmi Fiston Mayele hatakuwa sehemu ya kikosi cha Yanga kwa msimu wa 2023/24 baada ya kukamilisha dili lake la kujiunga na matajiri wa nchi ya Farao Pyramids ambao msimu huu watakuwa na kibarua kikubwa cha kulisaka taji la Ligi ya Mabingwa Afrika.
Mayele amekuwa na misimu miwili bora akiwa na kikosi cha Yanga aliyojiunga nayo akitokea AS Vita hadi anaondoka Yanga alifanikiwa kuweka shingoni medali saba, Ligi Kuu bara mara mbili, Ngao ya Jamii mara mbili, Kombe la Shirikisho la Azam mara mbili na medali ya mshindi wa pili kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Baada ya taratibu za Mayele kuondoka Yanga kukamilika mabingwa hao mara 29 wa Ligi Kuu Bara walimtambulisha straika wa zamani wa timu ya Bechem United, Hafidh Konkoni ambaye anatajwa kuja kurithi mikoba ya Predator Fiston Mayele.
Hakuna shaka yoyote Konkoni ni miongoni mwa washambuliaji bora na hilo limethibitishwa na takwimu zake akiwa na kikosi cha Bechem United licha ya timu hiyo kutokuwa na ubora kwenye michuano ya Caf lakini kwenye ligi ya ndani Konkoni ameonyesha makali yake.
Kufunga mabao 15 kwenye Ligi Kuu nchini Ghana si jambo dogo sote tunafahamu licha ya ligi nyingi za Ukanda wa Magharibi mwa Afrika kuwa na uchumi dhaifu lakini ni miongoni mwa maeneo ambayo yanazalisha wachezaji wengi wenye vipaji vikubwa na wengine tayari tunao kwenye ligi yetu.
Kitu pekee ambacho nataka kuwatahadharisha mashabiki na wapenzi wa Yanga waache muda uamue kwa Konkoni na wasianze kutengeneza ulinganisho na Mayele, mchezaji kusajiliwa ni jambo la kwanza na kufanikiwa kuonyesha alichonacho walau kwa asilimia sabini ni jambo jingine.
Ipo mifano mingi ya wachezaji wakubwa duniani ambao walikuwa miamba kwelikweli lakini walipohamia timu nyingine mambo yalikuwa magumu.
Hivyo Konkoni anaweza kuzoea mazingira haraka au achelewe kujipata kwa sababu ametoka kwenye ligi tofauti, utamaduni tofauti na mfumo mzima wa maisha pia ni tofauti na alipotoka hivyo haya yote yanaweza kuchangia kufaulu kwake ama kufeli kwake. Kuanza kumlinganisha na Mayele inaweza kumpa presha kubwa kwani hata yeye anajua ugumu uliopo mbele yake kutokana na mabalaa aliyoyaacha Fiston Mayele.
Malengo ya Yanga ni makubwa na yanahitaji wachezaji wakubwa kama Konkoni ambao wanaweza kuwafikisha Wananchi nchi ya ahadi yenye maziwa na asali hivyo wakati akiendelea kuzoea mazingira ajue kuna jukumu kubwa mbele yake na aliyekuwa kabla yake ameacha alama ambayo haiwezi kufutika kirahisi kwenye mioyo yao.
Maisha mapya bila Mayele Konkoni mchora ramani mpya kuelekea hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa. Kila la kheri Wananchi.