NGAO YA JAMII ANAPASUKA MTU LEO

LEO Jumapili kwenye Uwanja wa Wembley, Arsenal na Manchester City zinakutana kwenye mechi ya Ngao ya Jamii kuashiria kuanza kwa msimu mpya wa Ligi Kuu England.

Huu ni mchezo wa 115 wa Ngao ya Jamii unacheza tangu michezo hii ilipoanza kuchezwa mwaka 1908. Mchezo wa Ngao ya Jamii huzikutanisha timu bingwa wa Kombe la FA na Ligi Kuu England.

Manchester City ni bingwa wa Kombe la FA na pia ni bingwa ligi kuu. Hivyo Arsenal iliyomaliza nafasi ya pili kwenye Premier ndio imepata nafasi ya kucheza mchezo huo.

Hadi mwaka 2002 mechi hii ilikuwa ikifahamika kama Ngao ya Hisani lakini Tume ya Hisani iliikuta FA na hatia ya kuchelewa kupeleka fedha kwa jamii iliyohitaji hisani yao kutoka mauzo ya tiketi za mechi hii.

Kutokana na hali hiyo, mechi hii ikaitwa Ngao ya Jamii ili kuepuka tatizo hilo na Arsenal ilikuwa bingwa wa kwanza wa mechi hiyo baada ya kubadilishwa jina baada ya kuifunga Liverpool bao 1-0.

MECHI YA LEO

Katika mchezo wa leo utakaochezwa kwenye Uwanja wa Wembley, mwamuzi ni Stuart Attwell ambaye atasaidiwa na Tim Wood na Dan Robathan, mwamuzi namba nne ni John Brooks na mwamuzi msaidizi akiwa Steve Meredith.

ARSENAL

Wakati huu wa usajili kuelekea mechi ya leo, Arsenal chini ya Kocha Mikel Arteta imeimarisha kikosi chake kwa kuwasajili nyota watatu kwa bei za juu.

Kiungo Declan Rice ametua Arsenal majira haya ya joto kwa dau la pauni Milioni 105 wakiipiga bao Man City, Kai Havertz naye amesajiliwa kwa pauni 65m sambamba na beki Jurriën Timber aliyetokea Ajax kwa dau la pauni 38.6m pia wababe hawa wa London wako sokoni wakisaka mashine nyingine.

Katika mechi zake za kujiandaa na msimu ujao, Arsenal ilicheza mechi sita za kirafiki kati ya hizo ilishinda tatu, sare mbili na kupoteza moja.

Ilianza safari kwa sare ya 1-1 dhidi ya Watford, Nurnberg 1-1 Arsenal, MLS All-Stars 0-5 Arsenal, Man Utd 2-0 Arsenal, Barcelona 3-5 Arsenal.

Arsenal pia imetwaa ubingwa wa Emirates baada ya kuichapa Monaco kwa penalti 5-4 kufuatia sare ya bao 1-1 ndani ya dakika 90.

MAN CITY

Man City nayo wakati huu wa usajili haikuwa na mbwembwe kwani wamefanya usajili wa mchezaji mmoja ambaye ni kiungo Mateo Kovačić aliyetua kwa dau la pauni 25m kutoka Chelsea.

Katika kuandaa kikosi chake, Kocha wa City, Pep Guardiola amekiongoza kikosi chake kucheza mechi tatu za kirafiki kati ya hizo ameshinda mbili na kuchapwa moja.

City alianza pre season kwa kuichapa Yokohama F. Marinos mabao 5-3 kisha wakaipiga Bayern Munich 2-1 na mwisho wakachapwa wao mabao 2-1 na Atletico Madrid.

MACHO KWA HAALAND, RICE

Katika mchezo wa leo, watakaotazamwa sana ni Erling Haaland wa City na Rice wa Arsenal ambaye pia aliziingiza vitani klabu hizo kuwania saini yake na mwisho wa siku Gunners wakampata.

Leo itakuwa siku ya Rice kuwaonyesha Arsenal kuwa hawakufanya makosa kumsajili huku Haaland akipambana kuendeleza rekodi za kutupia mbele ya Washika Mitutu wa London.

HALI YA VIKOSI

Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta amethibitisha kumkosa Gabriel Jesus kutokana na kufanyiwa upasuaji wa goti pia atakosa baadhi ya mechi za awali za Premier League.

Mbali na Jesus, pia Bukayo Saka alikosa mchezo dhidi ya Monaco kutokana na homa lakini anaweza kuwa fiti kesho, huku Oleksandr Zinchenko ameendelea kuboresha afya yake japokuwa hajacheza hata dakika moja ya mechi za pre-season, kwahiyo inaweza kuwa ngumu kuanza leo.

Kwa upande wa City, kiungo Kevin De Bruyne ndiye mchezo pekee ambaye anaweza kukosa kutokana na kuuguza misuli ya paja tangu kwenye fainali ya Champions League Juni mwaka huu.

MAN UNITED KIBOKO YAO

Licha ya kutocheza mechi hii, Manchester United ndiyo klabu iliyotwaa mara nyingi zaidi ubingwa wa Ngao ya Jamii ikiwa imefanya hivyo mara 21.

Liverpool ndiyo inayofuatia ikiwa imefanya hivyo mara 16 sawa na Arsenal, Everton mara tisa, Tottenham Hotspur mara saba na Manchester City nayo mara sita.