MABOSI wa Chelsea wamekamilisha usajili wa beki, Axel Disasi kutoka Monaco kwa pauni milioni 40 kwa mkataba wa miaka sita.
Staa huyo pia alikuwa kwenye rada za Manchester United na Newcastle ambao pia walikuwa na nia ya kumsajili. Disasi aliweka wazi kuwa anatamani kushinda makombe na kufanya mambo makubwa akiwa Chelsea.
Akizungumza na tovuti rasmi ya klabu hiyo, Disasi alisema: “Ni jambo ambalo nimekuwa nikingojea. Nina furaha sana kuwa hapa, katika klabu hii kubwa. Ninajivunia sana kuwa sehemu ya familia hii kubwa, na ninatumai kufikia mambo makubwa sana hapa. Ili kushinda mataji. Nitafanya kila niwezalo kufikia malengo hayo.”
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 25 pia alizungumza kuhusu furaha yake ya kucheza mbele ya mashabiki wa Chelsea ambapo alisema: “Nina shauku ya kushuka uwanjani na kuhisi shangwe la mashabiki. Huu ni uwanja mzuri sana, ambao una ukaribu mzuri na mashabiki. Uwanja wa kawaida wa Kiingereza, nadhani.”
Wakurugenzi washiriki wa michezo wa Chelsea Laurence Stewart na Paul Winstanley walisema: “Axel ameonyesha ubora wake kwa misimu kadhaa nchini Ufaransa na hiyo imesababisha kutambuliwa kimataifa.”
“Yuko tayari kuchukua hatua inayofuata katika maisha yake ya soka na tunafuraha kuwa na Chelsea. Tunamkaribisha kwenye klabu na tunatazamia kuungana na Mauricio Pochettino na wachezaji wenzake wapya katika siku chache zijazo.”