NGUVU YA WASHKAJI INAKWENDA KUONEKANA MKWAKWANI TANGA

UKIONA giza linazidi wanasema kunakaribia kukucha, hivyo tu basi kwa namna joto la Ngao ya Jamii linavyozidi kukaribia basi ligi ipo njiani.

Waliotwaa taji ya Ngao ya Jamii 2022/23 ni Yanga wanakwenda kukutana na Azam FC. Timu zote zitakwenda kuonyesha nguvu ya ushikaji ndani ya Uwanja wa Mkwakwani Agosti 9.

Hapa tunakuletea baadhi ya mastaa watakaokuwa kwenye kazi ya nguvu:-

Sopu

Miguu yake ina zali anapokutana na Yanga iwe ni kwenye kufunga ama kutengeneza pasi za mabao. Katika mchezo wa ligi uliochezwa Uwanja wa Mkapa Septemba 6 2022 alitengeneza pasi ya bao moja dakika ya 65 mtupiaji akiwa ni Malicou Ndoye.

Baada ya dakika 90 ubao wa Uwanja wa Mkapa ulisoma Yanga 2-2 Azam FC.

Ahmada

Mbaya wake Feisal Salum aliyemtungua mabao mawili akiwa nje ya 18 Uwanja wa Mkapa hayupo ndani ya Yanga wamekuwa familia moja Azam FC.

Balaa la Fei atapishana nalo ikiwa atapewa nafasi ya kuanza kikosi cha kwanza ni kazi kuizuia michomo ya mtambo wa mapigo huru Aziz KI aliyekamilisha msimu wa 2022/23 akiwa na mabao 9 kibindoni na pasi tano za mabao kwenye mechi za ligi.

Feisal

Shuhuda wa timu ya Azam FC ikitunguliwa bao moja kwenye mchezo wa Azam Sports Federation fainali iliyochezwa Uwanja wa Mkwakwani, Tanga dhidi ya Yanga ikiwa ni muda mfupi baada ya kutambulishwa kwake.

Kazi inatarajiwa kuwa ngumu kwake atakapokutana na waajili wake wa zamani kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii hatua ya nusu fainali ya kwanza.

Bangala

Kasepa Yanga na dili la miaka miwili kasaini ndani ya Azam FC. Mchezo wake wa kwanza unatarajiwa kuwa dhidi ya mabosi wake wa zamani ambao ni Yanga Tanga.

Djigui

Kipa bora msimu wa 2022/23 akiwa na uzi wa Yanga hakuwa na bahati alipokutana na Azam FC mechi zote mbili nje ndani aliokota mabao mawili nyavuni.

Ule wa mzunguko wa kwanza ni mabao mawili alifungwa na mzunguko wa pili alifungwa mabao mawili. Sopu anaingia kwenye orodha ya mastaa waliomtungua mabao mengi kwenye mchezo mmoja ndani ya ligi ambayo ni mawili.

Anamkumbuka pia zama zile alipokuwa ndani ya Coastal Union kwenye mchezo wa fainali ya Azam Sports Federation alimtungua hat trick hiyo ilikuwa ni Julai 2 2022 mwisho Yanga ilitwaa taji hilo kwa ushindi wa penalty 4-1.

Lyanga

Mkali kwenye mapigo huru, Yanga hawana bahati naye kwenye mchezo wa mzunguko wa kwanza Uwanja wa Mkapa alitoa pasi ya kwanza kwa pigo huru dakika ya 23 kwa pigo huru na mtupiaji akiwa ni Daniel Amoah.

Bao la pili kwa Azam FC, Uwanja wa Mkapa kufungwa Lyanga alianza kupiga kona dakika ya 64 iliyokuwa chanzo cha bao kwenye mchezo huo.

Musonda

Kennedy Musonda alimpa tabu idrisu Abdulai kipa namba mbili wa Azam FC kwa kumtungua kwenye mchezo wa fainali ya Azam Sports Federation Uwanja wa Mkwakwani.

Ana ushikaji na kucheka na nyavu kibarua chake kwenye kete ya kwanza ya Ngao ya Jamii dhidi ya washikaji zake aliokutana nao msimu wa 2022/23 na wale aliokuwa nao ndani ya Yanga inaanza upya.

Job

Dickosn Job thamani ya tuzo ya beki bora wa msimu inakwenda kufunguliwa upya na kila shabaki akiwa na shauku ya kuona uwezo wake.

Ni mtu wa kazi msimu wa 2023/24 ataufungua kwa mguu upi ule wa kulia ama wa kushoto ni jambo la kusubiri na kuona itakavyokuwa.