Home Uncategorized SINGIDA BIG DAY HAWANA JAMBO DOGO/ JIBU LA MORRISON NA KAKOLANYA

SINGIDA BIG DAY HAWANA JAMBO DOGO/ JIBU LA MORRISON NA KAKOLANYA

MCHEZA kwao hutuzwa ipo hivyo na Singida Fountain Gate watakuwa nyumbani kuwapa burudani mashabiki wao ikiwa ni mwanzo kuelekea msimu mpya.

Agosti 2, 2023 ni sikukuu ya wakulima wa alizeti Singida Fountain Gate kwenye Uwanja wa Liti ikiwa ni Singida Big Day hii itakuwa sio ya mchezomchezo.

Hapa  tunakuletea namna mipango inavyokwenda Singida Fountain Gate:-

Mgeni rasmi

 Waziri wa Sanaa, Utamaduni na Michezo, Balozi Pindi Chana anatarajiwa kuwa mgeni Rasmi katika sikukuu ya Singida Big Day.

Ishu ya Morrison na Kakolanya

Timu hiyo inatajwa kuwa imekamilisha usajili wa nyota wawili ambao ni Bernard Morrison aliyekuwa anakipiga ndani ya Yanga pamoja na Beno Kakolanya aliyekuwa ndani ya Simba.

Wote hawa kwa sasa wapo huru na wanatajwa kumalizana na Singida Fountain Gate ikiwa madili yamejibu hatma yao itakuwa Uwanja wa Liti, Agosti 2.

Kete tano kwenye ratiba

Mpango kazi wa Singida Fountain Gate unabeba mambo mengi muhimu na miongoni mwa hayo ni yale matano yaliyopewa kipaumbele kikubwa ikiwa ni pamoja na utambulisho wa kikosi cha msimu wa 2023/24.

Ipo wazi kuwa wapo nyota wapya ndani ya kikosi hicho ikiwa ni pamoja na beki Joash Onyango ambaye alikuwa anakipiga ndani ya Simba, Yahya Mbegu huyu alikuwa Ihefu.

Wapo ambao wameboreshewa mikataba yao ikiwa ni pamoja na kiungo Bruno Gomes, Aziz Andambwile hawa wanatarajiwa kuwa kwenye utambulisho bila kumsahau Deus Kaseke pamoja na Meddie Kagere.

 Benchi la ufundi

Wachora ramani za ushindi ndani ya Singida Fountain Gate watakuwa hadharani kwa mashabiki ambapo kwa sasa timu hiyo inanolewa na Kocha Mkuu, Hans Pluijm.

Burudani kutoka kwa Wasanii

Singida Fountain Gate wanajua muziki ni furaha kwa mashabiki kama ilivyo mpira hawajaweka kando suala hili watakuwepo wasanii wakubwa kwenye tamasha lao.

Miongoni mwa wale ambao watakuwa jukwaani  ni pamoja na Nandy African Princess, Dulla Makabila mzee wa pita huku watakuwepo.

Mechi kali

Ni dhidi ya AS Vita hawa watakuwa wageni kwenye mchezo huo wa kimataifa katika kupimana nguvu ikiwa ni maandalizi ya kuelekea msimu mpya.

Mbali na mchezo huo mkali pia kutakuwa na mechi za utangulizi ambazo zitahusisha timu za Wanawake kwenye kutoa burudani.

Uzi mpya

Julai 19 2023 Singida Fountain Gate walitambulisha uzi mpya amao utatumika kwa msimu wa 2023/24.

Mbali na uzinduzi wa jezi mpya pia Singida Fountain Gate walizindua duka la klabu ambalo lina mahitaji muhimu ya timu hiyo inayoshiriki ligi.

Ofisa Habari wa Singida Fountain Gate, Hussein Massanza amesema kuwani sikukuu ambayo kila mtu anapaswa kuhudhuria kutokana na historia inayokwenda kuandikwa.

“Tunakwenda kuandika historia kubwa na itakayokumbukwa kwa wale ambao watahudhuria mipango inakwenda vizuri mashabiki wajitokeze kwa wingi.

“Kiingilio ni bei rafiki na hii itakuwa Uwanja wa Liti tunatambua kwamba wengi wanapenda kuona mambo mazuri hayo ni kwa ajili yetu hii sio ya mchezo mchezo.

“Mzunguko ni 3,000 na VIP ni 5,000 hili jambo linawezekana na tunajua  kwa ushirikiano kila kitu kitakwenda sawa,” amesema .

Previous articleSIMBA KUREJEA BONGO KUENDELEA NA KAZI
Next articleZAWADI MBALIMBALI KUTOLEWA NA “MERIDIANBET VUNA ZAIDI NA AIRTEL MONEY”