KIKOSI kipya cha Yanga kimeanza vizuri katika mechi yake ya kwanza kabisa kwa msimu mpya wa 2023/24 ikiwa ndio wanakionyesha kikosi chao wakati wa kilele cha tamasha la Mwananchi.
Bado hawajaanza mashindano rasmi lakini tayari angalau tumeona kikosi hicho kipya cha Yanga kinacheza namna gani.
Kocha Mkuu mpya wa Yanga, Miguel Gamondi ambaye ni raia wa Agentina na Italia, ame-diplay kikosi ambacho kinachohitaji au kitakuwa na soka la kazi.
Tumeona katika mechi yao dhidi ya Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini, Yanga waliibuka na ushindi wa bao 1-0 katika mechi ambayo Gamondi alitumia vikosi viwili.
Kikosi cha kipindi cha kwanza ambacho kilifanikiwa kupata ushindi wa bao hilo la ushindi na baada ya hapo akabadilisha kikosi kizima.
Kitu kizuri ni kwamba kikosi kilichoanza kikosi cha kwanza na kile kilichoingia kipindi cha pili, vyote vilikuwa na mrandano wa uchezaji.
Unaona aina ya kasi, timu inapokuwa inapanda na namna ya upangaji mashambulizi unafanana pia kama timu inapokuwa katika shape ya kulinda.
Hii maana yake kwa muda mfupi tayari Gamondi amefanikiwa kuendeleza shape ya kikosi alichokikuta kutoka kwa Nasredine Nabi lakini ameongeza vitu anavyovitaka yeye.
Ukikiangalia kikosi chake unaona hakuwa na haraka ya kutaka kubadilisha kila kitu, maana yake kikosi chake kinaweza kuendeleza mwendo.
Bila shaka, mashabiki wengi wa Yanga na wapenda soka au waelewa soka wamefurahishwa na namna kikosi cha Gamondi kilivyoanza ku-diplay licha ya kuwa na wachezaji wengi wapya.
Pamoja na hivyo nataka nikukumbushe, bado hatujaiona timu ya Gamondi katika mechi za mashindano dhidi ya timu za Tanzania. Kawaida mambo yanakuwa tofauti kidogo.
Hata kama ligi za nchi nyingine zimeendelea mfano wa Afrika Kusini lakini tukubali, ligi yetu ni ngumu na imepiga hatua kubwa sana kama utazungumzia suala la ushindani.
Hivyo Yanga itakapoanza kukutana na timu za Tanzania, si kweli kuwa kila kitu kitakuwa kama kilivyokuwa katika mechi dhidi ya Kaizer Chiefs. Ushindani utakuwa juu zaidi.
Pia ambacho tunapaswa kukumbuka kuwa wakati Gamondi anachukua kikosi, tayari Yanga imedondosha nyota wengi muhimu kwa sababu tofautofauti.
Djuma Shabani na Yannick Bangala wako kwenye mgogoro na klabu ya Yanga, wameweka msimamo wao kuwa hawataki kupelekwa kwa mkopo katika kikosi cha Singida Fountain Gate.
Hii imewatoa nyota hao katika kikosi cha Yanga na lazima tukubali kuwa kuna upungufu ambao utaanza kujengwa taratibu. Bangala alikuwa mchezaji bora wa Ligi Kuu Bara msimu mmoja uliopita. Djuma alikuwa beki bora wa kulia pia katika beki ya kulia.
Bernard Morrison licha ya kwamba hakuwa mchezaji tegemeo alikuwa na msaada wake. Ingawa nafasi yake pembeni kwa Yanga wanaonekana kuiziba vizuri.
Fiston Mayele ambaye uongozi wa Yanga umejaribu kufanya kila namna kuonyesha hakuwa wa mkopo jambo ambalo linaonyesha kuna shida kubwa katika kuutambua mpira na njia zake.
Mkopo si dhambi lakini yale maneno ya mwanzo mbele ya Wanayanga kuwa si wa mkopo, sasa inakuwa ni kama aibu kusema ni wa mkopo. Lakini ukweli ni wa mkopo na jibu unalipata sasa, kuwa mchezaji una mkataba naye hadi 2024, lakini kwenye kutambulishwa hakwenda na alikuwa nyumbani kwake jijini Dar es Salaam.
Wakati nakuachia hilo ufikirie, acha turudi katika hoja ya msingi kuwa Gamondi atamkosa mtu kama Mayele pia. Mshambuliaji ambaye amekuwa mfungaji bora wa pili na wa kwanza katika misimu miwili ya ligi kuu lakini mfungaji bora wa misimu yote katika kikosi chake.
Gamondi anaingia Mayele anaondoka. Maana yake kuna kitu taratibu kitatakiwa kujengwa na huenda kupitia Kennedy Musonda ambaye pia bado atahitaji muda kidogo.
Mashindano yatakapoanza bado kutakuwa na vitu vya kujifunza kwa kocha huyo. Na ukumbuke si kila mechi itachezwa kwenye dimba la Mkapa.
Taratibu ataanza kujua ugumu wa ligi, naye ataanza kujipanga afanye lipi na nini cha kupunguza na kuongeza.
Gamondi ni kocha anayefanya kazi kwa mara ya kwanza katika Ukanda wa Afrika Mashariki. Maana yake kuna mambo atatakiwa pia kujifunza katika soka la ukanda huu.
Ukiachana na hilo, pia usisahau kuwa Yanga ilikuwa timu inayofungika kwa shida katika misimu hii miwili. Imekwenda na rekodi ya kutofungwa kwa muda mrefu na hizi zote zinaweza kugeuka kuwa presha kwa kocha huyo kama itafanya vibaya kidogo tu.
Kufanya vibaya ikiwa ni mara mbili tatu halafu mashabiki wakashindwa kutulia na viongozi wakashindwa kuibeba hiyo presha maana yake, kafara atakuwa Gamondi.
Ndio maana nikasema lazima kuwe na uvumilivu na hasa kama itatokea hali hiyo. Uvumilivu una mwisho wake lakini lazima uwepo angalau hata kama ni kwa kiasi fulani.
Utakapokosekana uvumilivu, maana yake kutakuwa na hali ya makocha wapya ingia toka ambayo wakati mwingine inaweza kuwa athari zaidi kwa Yanga ambayo imekuwa na kipindi bora kwa misimu miwili iliyopita.