UONGOZI wa Simba umefafanua mbinu ilizotumia kuinasa saini ya kiungo Fabrice Ngoma ambaye alikuwa anatajwa kuwa kwenye hesabu za watani zao wa jadi, Yanga.
Nyota huyo aliyekuwa anakipiga Al Hilal ya Sudan alitambulishwa na Simba Julai 14 na alisaini dili la miaka miwili kuitumikia timu hiyo inayonolewa na Kocha Mkuu, Roberto Oliveira.
Yanga wanatajwa kuwa walikuwa kwenye hesabu za kuinasa saini ya nyota huyo wakapishana naye.
Pia inatajwa kwamba Yanga walikuwa kwenye hesabu za kuinasa saini ya kiungo Clatous Chama aibukie Jangwani Simba wakakaa mezani na Chama kabla hajamalizana na Yanga.
Kwa sasa wachezaji hao wote wawili wapo Uturuki kwa maandalizi ya msimu wa 2023/24.
Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba, Ahmed Ally amesema kuwa waliibuka Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Nyerere usiku kumpora mchezaji huyo ambaye alikuwa anahitajika na timu nyingi Afrika.
“Simba tumeingia airport tukauliza anashuka saa ngapi tukaambiwa saa 9:30 usiku aliposhuka tukaona wamekaa kizembe tukamchukua, wakaanza kupiga kelele mchezaji wetu mchezaji wetu sisi hatukujali.
“Kama hakuwa mchezaji ambaye walikuwa wanamtaka walifuata nini airport? Hapa ni ubayaubaya mchezaji alichagua kwenda Uturuki sisi tunasema mchezaji yeyote watakayemshusha airport tutamchukua labda wabadili aina ya usafiri,” amesema Ahmed.