KAZI YA USAJILI IFANYIKE KWA UMAKINI MKUBWA

TAYARI kazi ipo wazi kwa sasa kutokana na dirisha la usajili kufunguliwa Julai Mosi na Agosti 31 dirisha la usajili linatarajiwa kufungwa.

Kuanzia Championship, Ligi ya Wanawake, First League mpaka NBC League tayari wana taarifa kwamba dirisha la usajili lipo wazi.

Sio Yanga, Singida Big Stars ambayo kwa sasa ni Singida Fountain Gate FC ni muhimu kuwa na mipango makini.

Mpaka Geita Gold bila kusahau Namungo FC jambo la msingi ni umakini kwenye usajili mpaka KMC.

Huu ni muda ambao timu zinapaswa kutulia na kufanya kazi kwa umakini kwenye kutafuta ushindi kwenye kuwapata wachezaji ambao wanawahitaji.

Sio jambo dogo kushinda kwa kufanya usajili makini kwa kuwa kila mchezaji anayetafuta nafasi ya kupata mkataba lazima avutie kwake.

Mawakala nao wamekuwa wakiwapamba wachezaji wao kwa kutengeneza wosifu mzuri ambao ni moja ya sababu zinazofanya wapate timu mpya lakini umakini unahitajika.

Kwa sasa sio muda wa kuanza kupambana kugombania wachezaji ilihali wachezaji wenye uwezo mkubwa wapo kila kona kikubwa ni umakini kwenye uchaguzi wa wachezaji.

Wale ambao wamepewa jukumu la kusajili wachezaji ni muhimu kufanya mawasiliano na benchi la ufundi na kutumia ripoti katika kuboresha kikosi.

Zile ambazo zimepanda ikiwa ni pamoja na Mashujaa kutoka Kigoma wanapaswa kutambua kwamba mwisho wa kupata matokeo ndani ya ligi ni pale uwekezaji unapokuwa mdogo.

Ligi inahitaji uwekezaji mkubwa na ni muhimu kila mmoja kuwekeza kwenye kila idara kuanzia benchi la ufundi pamoja na wachezaji uwanjani.

JKT Tanzania hawa angalau wana uzoefu walishawahi kuonja ladha ya kushiriki ligi lakini wakianguka tena kwenye uwekezaji ni rahisi kurejea kule walikotoka.