Home Sports BEKI JOASH ONYANGO APEWE ULINZI

BEKI JOASH ONYANGO APEWE ULINZI

MZUNGUKO wa dunia unavyozidi kwenda na matukio yanaongezeka na kwenye ulimwengu wa mpira kila wakati kumekuwa kuna mabadiliko ambayo yanatokea.

Ndani ya kikosi cha Simba kuna beki wa kazi Joash Onyango ambaye amekuwa akionekana kwenye uvurugaji mara nyingi jambo linalowavuruga mashabiki pamoja na viongozi kwamba asepe ama abaki.

Licha ya yote hayo beki huyo anahitaji kupewa ulinzi na uzoefu wake kwenye mechi za kitaifa na kimataifa unampa nguvu ya kuendelea kuonyesha makeke yake.

Hapa tunakuletea makeke yake akiwa na uzi wa Simba namna hii:-

Rekodi yake imetibuliwa

Msimu wa 2021/22 alicheza mechi 23 akisepa na dakika 1,887 uwanjani kwenye kupambania nembo ya uzi wa Simba yenye maskani yake pale Msimbazi na alitupia bao moja kibindoni.

Msimu wa 2022/23 rekodi yake imetibuliwa akiwa na deni la mchezo mmoja kuvunja rekodi yake mwenyewe akiwa amecheza mechi 22.

Ni dakika 1,739 kayeyusha uwanjani akiwa hajafunga bao wala kutoa pasi ndani ya msimu huu ambao Simba hawajasepa na taji lolote kibindoni.

Kimataifa kaweka rekodi yake

Kwenye anga za kimataifa katika mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika eki huyo ameandika rekodi yake msimu huu kutokana na kupambana kuokoa hatari huku akisababisha penalti.

Ilikuwa Februari 11 dhidi ya Horoya ugenini alisababisha penalti dakika ya 70 mikono ya Aishi Manula iliokoa na alionyeshwa kadi ya njano dakika ya 70 katika mchezo huo.

Katika mchezo wa hatua ya makundi mwingine ilikuwa dhidi ya Raja Casablanca, Uwanja wa Mkapa Februari 18 kwenye mchezo huu Onyango alisababisha penalti dakika ya 85 na Ismael Mokadem dakika ya 86 alimtungua Manula.

Walipokutana na Raja ugenini Uwanja wa Mohamed V alisababisha penalti dakika ya 68 ikazamishwa kimiani na Khamza Khabba ilikuwa ni dakika ya 70.

Onyango ni miongoni mwa mabeki wa Simba walioiongoza timu hiyo kutinga hatua ya robo fainali.

Wydad wanalijua balaa lake

Katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa hatua ya robo fainali uliochezwa Uwanja wa Mkapa, Simba ilipata ushindi wa bao 1-0 huku ukuta wa Simba haukuruhusu bao.

Katika dakika 90 za awali Uwanja wa Mkapa Onyango alikuwa sahani moja na mabeki wa Waydad ambao walikwama kumtungua kipa namba tatu wa Simba Ally Salim.

Ngoma ilikuwa nzito ugenini kosa moja katika harakati za kuokoa mpira ngoma ikazamishwa kimiani baada ya jitihada za Salim kukwama kuokoa hatari hiyo.

Anafuta makosa yake

Rekodi zinaonyesha kwenye kwenye mchezo dhidi ya Yanga uliochezwa Uwanja wa Mkapa Novemba 7 2020 alisababisha faulo iliyoleta penalti.

Ngoma ilikuwa dakika ya 28 kwenye harakati za kuokoa hatari kwenye miguu ya Tuisila Kisinda nje kidogo ya 18 alimchezea faulo na mwamuzi akaamuru iwe penalti na akaonyeshwa kadi ya njano, mtupiaji kwa Yanga alikuwa ni Michael Sarpong aliyemtungua Aishi Manula.

Ni yeye alifuta makosa yake kwenye mchezo huo dakika ya 85 alipopachika bao kwa kichwa akitumia pigo la kona lililopigwa na kiungo Luis Miquissone na kuwafanya wagawane pointi mojamoja kwenye mchezo huo na kufuta makosa yake.

Kwenye ligi wamoto

Ukuta wa Simba wenye Henock Inonga, Mohamed Hussein, Shomary Kapombe, Kennedy Juma ni namba moja kwa timu ambazo zimefungwa mabao machache.

Baada ya kucheza mechi 30 ni mabao 17 Simba imefungwa huku ikiwa imetunguliwa bao moja kwa mkwaju wa penalti ilikuwa dhidi ya Coastal Union.

Ikumbukwe kwamba sio Onyango ambaye alisababisha penalti hiyo ni beki wa mtumba Kennedy.

Imeandikwa na Dizo Click na kutoka gazeti la Championi Jumatano.

Previous articleVIDEO:SABABU YA YANGA KUMPA KAZI KOCHA IBENGE
Next articleCR 7 KAANDIKA REKODI NYINGINE