>

KOCHA YANGA AWEKA UGUMU HUU

KOCHA Msaidizi wa Yanga, Mrundi Cedric Kaze amekataa kusaini mkataba mpya wa timu hiyo, akitoa masharti magumu kwa uongozi ulioanza mazungumzo ambao ulitarajiwa kukutana naye mapema.

Mkataba wa Nabi na Kaze ulimalizika Jumatatu hii mara baada ya mchezo wa Fainali ya Kombe la FA kumalizika kwa Yanga kutwaa taji hilo kwa kuwafunga Azam FC bao 1-0 lililofungwa na Kennedy Musonda uliopigwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.

Mmoja wa Mabosi wa Kamati ya Utendaji ya Yanga ameliambia Championi Ijumaa kuwa mazungumzo yalishindwa kufikia muafaka mzuri kati ya uongozi na Kaze ambaye ameomba afanyiwe maboresho katika mkataba wake mpya.

Bosi huyo alisema kuwa kikubwa ameutaka uongozi wa timu hiyo, kuongeza ofa ya kuongeza mkataba na mshahara ambayo ni siri aendelee kubakia hapo Jangwani.

Aliongeza kwa kutoa sharti la kuchukua dau hilo la kumbakisha na mshahara huo, lakini awe kocha mkuu na sio msaidizi kama ilivyokuwa awali.

“Mara tu baada ya kuondoka kwa kocha Nabi, viongozi wamefanya mazungumzo na kocha msaidizi Kaze ili aongeze mkataba mpya.

“Katika mazungumzo hayo, kocha huyo amegomea ofa aliyopewa na uongozi wa Yanga ameomba aongezewe zaidi au ibaki hiyo hiyo ila awe kocha mkuu na sio msaidizi tena.

“Kwani tayari ana ofa nyingine nyingi alizopewa kwa ajili ya msimu ambazo kutoka ndani na nje ya nchi, hivyo kama akishindwana basi ataondoka,” alisema bosi huyo.

Meneja wa Habari na Mawasiliano wa timu hiyo, Ally Kamwe alizungumzia hilo kwa kusema kuwa: “Bado mazungumzo yanaendelea kati ya uongozi wa klabu na Kaze pamoja na watumishi wengine ambao mikataba yao imemalizika.”