>

SIMBA KUNA UMUHIMU KUBORESHA ENEO LA MLINDA MLANGO

MAKOSA ya Salim Juma ni yaleyale ndani ya dakika 180 ambazo amefungwa kwenye mechi mbili za Ligi Kuu hivi karibuni.

Kipa huyo alipewa majukumu kwenye mechi kubwa pia ikiwa ni dhidi ya Yanga ambapo hakufungwa.

Ikumbukwe kwamba Yanga ni mabingwa wa ligi msimu wa 2022/23 huku Simba wakigotea nafasi ya pili.

Mchezo dhidi ya Namungo bao alilotunguliwa na Hassan Kibunda ni pigo la kona mpira ulikuwa juu ulimshinda katika harakati za kuokoa ngoma ikajaa nyavuni.

Dhidi ya Polisi Tanzania pigo la kona kwenye harakati za kuokoa ngoma ikazama nyavuni dakika ya 85.

Kuelekea kwenye maboresho ya kikosi cha Simba ni muhimu kuangalia na eneo la mlinda mlango ambalo akipata maumivu Aishi Manula hali inakuwa tofauti hakuna mbadala wake.

Beno Kakolanya yupo lakini naye hapewi nafasi kuonyesha uwezo wake huku akitajwa kuwa kwenye hesabu za kusepa ndani ya kikosi cha Simba msimu ujao.

Mchezo wa kukamilisha msimu kwa Simba unatarajiwa kuchezwa Juni 9 itakuwa dhidi ya Coastal Union ya Tanga huku Salim akipewa nafasi kubwa ya kuanza kikosi cha kwanza.

Manula ambaye ni kipa namba moja wa Simba yupo Afrika Kusini akipewa matibabu baada ya kupata maumivu kwenye mchezo dhidi ya Ihefu ambao ulikuwa ni wa Kombe la Azam Sports Federation.