RUVU SHOOTING TUTAONANA BAADAYE, KUNA KUSHUKA DARAJA

  NI rasmi timu ya Ruvu Shooting imeshuka daraja na haitakuwa sehemu ya timu za Ligi Kuu Bara kwa msimu wa 2023/24 huku timu za Polisi Tanzania, Mtibwa Sugar na KMC zikipambania hatma yao kwenye michezo miwili waliyobakisha kumaliza ligi.

  Kwa misimu ya hivi karibuni Ligi Kuu Bara imekua na ushindani mkubwa ambapo uwekezaji mkubwa uliofanywa na Azam Media pamoja na benki ya NBC kwa kiasi kikubwa umeleta tija kwenye ligi yetu.

  Kwa sasa hakuna zile stori za timu kukosa nauli, kuzuiwa hotelini au timu kushindwa kulipa mishahara hivyo suala hili kwa kiasi kikubwa limeongeza ushindani kwenye ligi yetu jambo lililopelekea Ligi Kuu Bara kuwa miongoni mwa ligi 10 bora Afrika kitu ambacho hatukuwahi kukiona hapo awali.

  Timu za Kitayosce (Tabora United) na JKT Tanzania rasmi zimejihakikishia nafasi yao msimu ujao na zitakuwa miongoni mwa timu za ligi kwa msimu wa 2023/24 baada ya kumaliza kwenye nafasi mbili za juu kule Championship, JKT wakimaliza mabingwa na Kitayosce wakimaliza kwenye nafasi ya pili.

  JKT Tanzania si mara yao ya kwanza kuwa sehemu ya timu za Ligi Kuu Bara na kwa upande wa Kitayosce wao wanaonja ladha ya ligi kwa mara ya kwanza baada ya msimu uliopita kushindwa kupanda.

  Kama mlivyofanikiwa kupanda daraja pia kumbukeni kuna kushuka kama hamtajipanga. Kuna tofauti kubwa kati ya Ligi Kuu Bara na Championship kuanzia aina ya wachezaji, mipango ya mechi (game approach) na aina ya makocha hivyo msichanganye madesa hapa.

  Timu za Njombe Mji, Mbeya Kwanza, Ihefu FC, Mgambo JKT, African Sports hizi ni baadhi ya timu ambazo ziliwahi kucheza ligi kwa msimu mmoja na msimu uliofuata walirudi walipotoka baada ya kuja kwenye ligi mipango ya Championship hivyo JKT Tanzania na Kitayosce mnapaswa kulizingatia hili.

  Huu ndiyo muda wenu wa kufanya maboresho makubwa kwenye vikosi vyenu na mabenchi ya ufundi pia kwenye eneo la utawala viongozi huu ni muda wenu kuhakikisha mnatengeneza mipango mikakati ya kuzifanya timu zenu kuwa tishio kuelekea msimu mpya wa mashindano ili tuendelee kuwa na ligi bora na yenye ushindani.

  Timu za Pamba na Mashujaa FC wana nafasi ya dhahabu kuitafuta nafasi ya kucheza Ligi Kuu Bara msimu ujao ambapo timu hizi zitacheza Playoff na mshindi atacheza mchezo wa mtoano na moja ya timu itakayomaliza kwenye nafasi ya 13 na 14 kwenye Ligi Kuu Bara.

  Hivyo mkizichanga karata zenu vizuri mna nafasi ya kuongeza idadi ya timu za Ligi Kuu Bara msimu ujao kila la kheri kwenu. Kwa upande wa timu ya Polisi Tanzania ni miujiza pekee inayohitajika ili kuweza kuwanusuru na janga la kushuka daraja ambapo wanahitaji kushinda mechi zao zote zilizobaki ili kusogea walau kwenye nafasi ya kucheza playoff na kufufua tumaini la kusalia kwenye ligi kwa msimu ujao.

  Wanahitaji ushindi kwenye mechi dhidi ya Simba SC na Azam FC ili kuamua hatma yao ya kubaki kwenye ligi.

  Ligi Kuu Bara si lele mama inahitaji kujipanga kwenye kila idara ili uweze kuwa bora uwanjani, unaweza kuwa na kikosi imara lakini kama hakuna mipango thabiti na uongozi bora si ajabu kuona timu inashuka daraja hivyo mnatakiwa kujipanga ili kuwa bora. Kila la heri JKT Tanzania na Kitayosce kwaheri wazee wa PTK Ruvu Shooting ya mwalimu Masau Bwire.

  Previous articlePOLISI TANZANIA YAGOMEA KUSHUKA DARAJA
  Next articleMAYELE ATIKISA AFRIKA,MBRAZIL SIMBA ATANGAZA BALAA ZITO