KIMATAIFA YANGA MMEFANYA KAZI KUBWA, SIMBA PIA

HAKIKA ni wakati mzuri kwa Yanga kutokana na kile ambacho walikuwa wanapigia hesabu kujibu kwa wakati.

Kutinga hatua ya nusu fainali kwenye mashindano makubwa Afrika ni heshima kwa Tanzania na timu yeyewe inaonyesha ukomavu wake.

Wachezaji bila kusahau benchi la ufundi hakika walikuwa kwenye kazi kubwa kutimiza majukumu yao uwanjani na nje ya uwanja.

Mashabiki wamepokea kwa furaha matokeo ya Yanga. Tanzania imefurahi na kila mmoja anaona namna ilivyo raha pale porojo zinapokwekwa kando kisha kazi ikafanyika.

Haya yote hayajatokea kwa bahati mbaya bali ni uwekezaji na kukubali kujifunza pale ambapo inatokea makosa yanafanyika.

Kuwa kwenye hatua ya nusu fainali inamaanisha kwamba Afrika inatambua ukija Tanzania kuna timu kubwa ikiwa ni pamoja na Yanga ambayo imetinga hatua ya nusu fainali.

Pongezi kwa wachezaji na mnapaswa kuendelea kufanya kazi ikiwa lengo la kutinga nusu fainali limewezekana basi hata fainali pia inawezekana.

Kwa Simba juhudi kubwa kwa wachezaji zimeonekana na kushindwa kusonga hatua ya nusu fainali ni somo kubwa ambalo sasa linapaswa kufanyiwa kazi kwa vitendo.

Hatua kubwa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika na ni dhidi ya timu kubwa ambayo mmeshinda mlipokuwa nyumbani kisha ugenini maamuzi ya penalti yakatoa mshindi wa mwisho.

Wakati ujao tunaamini utakuwa bora kwenu na mtafanya kazi kubwa ambayo itawapa matokeo mazuri kwa makosa ambayo mmefanya.

Pongezi kwenu  na mashabiki kwa namna ambavyo wamekuwa wakijitoa kuona timu inapata matokeo mazuri, wakati ujao tunaamini mtakuwa bora zaidi.