MWENYEKITI wa Tawi la Yanga, Gerezani, Kariakoo, Hassan Sasama amesema kuwa mashabiki wa Yanga wajitokeze kwa wingi Uwanja wa Mkapa kulipa kisasi mbele ya Rivers United katika mchezo wa hatua ya robo fainali dhidi ya Rivers United.
Yanga ina kibarua cha kusaka ushindi dhidi ya Rivers United ikiwa ni robo fainali ya pili wana faida ya mabao 2-0 waliyopata ugenini ambapo mabao yote yalifungwa na Fiston Mayele.
Sasama amesema:”Kutokana na umuhimu wa mechi hii mashabiki tujitokeze kwa wingi kwa kuwa tunakwenda kuandika rekodi ya kutinga hatua ya nusu fainali Kombe la Shirikisho Afrika, ushindi wetu ugenini haina maana kazi imekwisha.
“Bado kazi inaendelea ni wakati wa kujitokeza na kushangilia muda wote sio muda timu ikiwa na mpira,tujae kwa wingi kulipa kisasi,” amesema Sasama.
Twaha Chegeka ambaye ni mlezi wa Tawi la Yanga Gerezani amesema:-“Hii ni timu ya Wananchi wote tayari kisasi namba moja tumelipa kwa kuwa walitufunga mabao mawili na kutuondoa katika Ligi ya Mabingwa Afrika sasa tunataka kuwaondoa katika Kombe la Shirikisho Afrika,”.
Rashid Mandwanga amesema kuwa katika dakika 180 ni dakika 90 zimechezwa bado 90 hivyo Watanzania wajitokeze kwa wingi kumaliza dakika 90 zilizobaki.
Saleh Bachu mwanachama wa Tawi la Yanga Gerezani amesema kuwa kukutana na Rivers ni bahati kwa kuwa waliwafunga katika Ligi ya Mabingwa Afrika hivyo kazi yao ni kulipa kisasi.