SIMBA YATAMBIA MFUMO WAKE

ROBERTO Oliveira, Kocha Mkuu wa Simba amesema kuwa timu hiyo inacheza mchezo wa kisasa jambo linalowapa matokeo kwenye mechi ambazo wanacheza kitaifa na kimataifa.

Simba imecheza jumla ya mechi 19 mfululizo za ligi bila kupoteza na timu ya mwisho kuifunga ilikuwa ni Azam FC mtupiaji akiwa ni Prince Dube Uwanja wa Mkapa.

Kwenye mechi nne mfululizo ambazo ni dakika 360 Simba haijapoteza ilikuwa ikishinda mechi zote ikiwa ni Simba 5-1 Ihefu mchezo wa Kombe la Shirikisho hatua ya robo fainali,Ihefu 0-2 Simba mchezo wa ligi,Simba 2-0 Yanga mchezo wa ligi.

Wakati ubao wa Uwanja wa Mkapa ukisoma Simba 1-0 Wydad Casablanca, mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya robo fainali hapo aligotea kwenye mchezo wa nne bila kufungwa kwenye mechi za ushindani.

Akizungumza na Spoti Xta, Oliviera alisema kuwa wanatambua namna ya kupambana na wapinzani wao kitaifa na kimataifa kutokana na mbinu za mpira wa kisasa kukubalika kwa wachezaji wake.

“Unaona ambavyo tunacheza kwenye mechi zetu iwe ni mechi za kitaifa na kimataifa ni mtindo wa kisasa ambao tunatumia unatupa matokeo chanya na hili ni furaha kwetu.

“Pongezi kwa wachezaji kutokana na kujituma kwao na wanafanya kazi nzuri ninawapongeza, bado tuna kazi nyingine kwenye mchezo wetu ujao dhidi ya Wydad ambapo tutakuwa ugenini.

“Kwenye mpira kila kitu kinawezekana ni suala la kusubiri na kuona hasa kwenye kutengeneza nafasi na kutumia, mpira ni mchezo ambao unaangalia mpira upo na nani na atafanya nini kwa wakati huo,” amesema Oliveira.