ROBERTO Oliveira, Kocha Mkuu wa Simba amesema uwepo wa nyota kama Clatous Chama, Saido Ntibanzokiza, Kibu Dennis pamoja na wachezaji wengine wote wa Simba unampa nguvu ya kuamua nani ataanza kikosi cha kwanza na kupata matokeo.
Ni dakika 1,710 ambazo ni mechi 19 mfululizo za ligi kocha huyo akishirikiana na Juma Mgunda wameongoza bila kufungwa baada ya kupoteza dhidi ya Azam FC walipofungwa bao 1-0.
Amepata ushindi dhidi ya Yanga wa mara ya kwanza akiwa kwenye benchi la ufundi ndani ya timu hiyo yenye maskani yake Msimbazi.
Kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika kocha huyo amekiongoza kikosi hicho kupata ushindi dhidi ya Wydad Casablanca ambao ni mabingwa watetezi.
Ikiwa na mtaji wa bao moja kibindoni inatarajiwa kucheza na Wydad Aprili 28 nchini Morocco kwenye Uwanja wa Mohamed V.
Oliveira amesema kuwa kuna wachezaji wazuri kwenye kikosi cha Simba ambao wanafuata maelekezo wanayopewa jambo linalompa furaha.
“Ninafurahi kuwa ndani ya Simba kuna wachezaji wengi wenye uwezo mkubwa ikiwa ni pamoja na Clatous Chama, Saido Ntibanzokiza, Jean Baleke, Kibu Dennis, Mohamed Hussein, Joash Onyango.
“Wote wanacheza kwa ushirikiano na hili ni jambo la muhimu kwetu kuona tunapata matokeo mazuri na kushinda mechi ambazo tunacheza tunaamini tutafanya vizuri kwenye mechi zetu ambazo zinatukabali,” amesema Oliveira.