BALEKE, MAYELE WAPEWE TU MAUA YAO

    “WASHA Wifi na usizime Data, hawa ni Wekundu wa Msimbazi Simba, wanaendelea palepale walipoishia, Jean Baleke namna ambavyo anafanya, ndivyo ambavyo anaendeleza kwenye Dimba la Benjamin Mkapa,” alisikika akiunguruma mtangazaji wa kituo cha ZBC2, Ghalib Mzinga akisherehesha bao la Baleke dhidi ya Wydad Casablanca.

    Ndiyo, Jumamosi iliyopita kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam wawakilishi wa Tanzania katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika Simba walifanikiwa kupata ushindi muhimu wa bao 1-0 dhidi ya mabingwa watetezi Wydad Casablanca katika mchezo wa mkondo wa kwanza wa robo fainali ya mashindano hayo.

    Kwa yoyote anayeifuatilia vizuri Wydad Casablanca na utofauti wa madaraja ya kiuwekezaji kwenye soka kulinganisha na Simba basi atakubaliana nami kuwa Simba wanastahili pongezi kubwa.

    Kama ilivyokuwa kwa Simba, siku ya Jumapili watani zao wa jadi Yanga nao walifanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya wenyeji wao Rivers United ya Nigeria. Pongezi nyingi kwa mabao mawili ya straika Mkongomani, Fiston Mayele.

    Mabao hayo yamemfanya Mayele kufikisha idadi ya mabao 50 tangu atue Yanga katika kipindi cha muda mfupi wa misimu miwili tu, tena huu wa pili ukiwa bado unaendelea na kuna nafasi kubwa ya idadi hiyo kuongezeka.

    Huko kwenye mtandao wa kijamii wa YouTube kuna nyimbo ya msanii maarufu Mwanaharakati inaitwa ‘Nipeni Maua Yangu’, nadhani kwa kazi iliyotukuka inayoendelea kufanywa na Yanga na Simba kupitia Baleke na Mayele basi wanastahili kupewa maua yao.

    Hiki kinachofanywa na Simba sio kitu kidogo kama ambavyo wengi wetu tunakichukulia katika hali ya mazoea, ni kitu kigumu sana kuwa na timu mbili katika hatua ya robo fainali ya mashindano ya klabu Afrika, ukitaka kuamini fuatilia kuona ni nchi ngapi zimefanikiwa kufanya hivyo.

    Baada ya pongezi hizo turudi kwenye jambo la msingi, ikumbukwe matokeo ya michezo hiyo ya mkondo wa kwanza ni kama kumalizika kwa dakika 45 za kwanza tu za mchezo, na kuna kazi kubwa ya dakika 45 za pili yaani michezo ya marudiano.

    Ni kweli haya mmeanza vizuri sana lakini kuna wakati napenda kuwakumbusha watu miongoni mwa kauli maarufu iliyowahi kutamkwa na Mwanafalsafa kuwa ‘haijaisha, mpaka iishe’.

    Kauli hii ina mlengo wa kueleza haipaswi kudhania kazi imeisha ikiwa nusu, hata kama ina mafanikio makubwa au madogo kiasi gani.

    Kuna wakati aliyewahi kuwa Msemaji wa Yanga Haji Manara kupitia jukwaa la akaunti yake rasmi ya mtandao wa kijamii wa Instagram kabla ya kucheza dhidi ya Al Hilal ambapo aliandika ujumbe ulioleza kuwa atakuwa mtu wa mwisho kuamini safari imeisha kufuatia matokeo mabaya ya hapa nyumbani.

    Hivyo tukumbuke ni mapema sana kuona imeisha bali ndo kwanza safari inaanza na wanapaswa kurekebisha wapi walipokosea na kuuongeza ufanisi kutokana na mazuri.

    Ikumbukwe kufanya vizuri huku kwa Simba na Yanga ni heshima sio kwa sekta ya michezo pekee, bali kwa Taifa kwa ujumla na ndio maana hata Serikali imeona haja ya kuweka nguvu, ambapo Rais Dk Samia Suluhu kupitia idara ya mawasiliano Ikulu wanaendelea na motisha ya kununua kila bao moja kwa Shilingi Milioni tano.

    Tukapambane kwa ajili ya heshima ya Simba na Yanga, lakini kwa umuhimu mkubwa zaidi tukapambane kwa ajili ya heshima ya nchi. Nusu finali kwa timu mbili zinawezekana lakini lazima vitendo vihusike.

    Previous articleMBEYA CITY HAWAJAKATA TAMAA
    Next articleWASHIKA BUNDUKI MAMO MAGUMU, CITY WAPIGA 4G