MECHI dume kabisa, mechi ya kibabe na mechi ya kibingwa inapigwa leo pale Dimba la Etihad, wana wanakwambia mshindi wa leo anaasilimia kubwa ya kuwa bingwa wa Premier League msimu huu.
Leo Jumatano Manchester City chini ya Kocha Pep Guardiola itaikaribisha Arsenal kwenye Uwanja wa Etihad katika mchezo wa Ligi Kuu ya England ambao unatarajia kutoa picha ya ubingwa msimu huu.
Matokeo yoyote katika mchezo huu yana maana kubwa sana hususan kwa timu hizo. Arsenal ambao wako kileleni wakiwa na alama 75 watakuwa wanapambana kutafuta pointi tatu dhidi ya City ambao wako nafasi ya pili na alama zao 70.
Vita kubwa iko nafasi mbili za juu, hapo ndipo bingwa anatokea msimu huu. Arsenal waliongoza ligi kwa muda mrefu kabla ya kuyumba kwa kutoa sare tatu mfululizo.
Arsenal wamekuwa wakiteleza taratibu katika mbio za kuwania taji la Premier baada ya kuporomoka pointi katika mechi tatu mfululizo, huku sare ya 3-3 Ijumaa iliyopita ikiwaweka kwenye wakati mgumu zaidi wa kufanikisha malengo yao.
Matokeo hayo yanafanya mambo kuwa mabaya zaidi kwa vijana wa Mikel Arteta, ambao waliongoza kwa pointi nane zaidi mwanzoni mwa mwaka ikilinganishwa na tano pekee kwa sasa.
Kikosi hicho cha London Kaskazini kimecheza michezo miwili zaidi ya Man City. Cha kufurahisha ni kwamba mechi yao ya leo inaongeza mvuto zaidi kuitazama kwani ushindani unatarajiwa kuwa mkali.
Kama City atashinda mechi ya leo basi atafikia pointi 73 na mchezo mmoja mkononi, kama akishinda na huo anatulia kileleni, ugumu wa mechi unaanza hapa nani atakubali kuwa daraja kwa mwenzake?
FOWADI ZAO VIWEMBE, BEKI CITY KALI
Takwimu zinaonyesha fowadi ya klabu zote ziko imara kwani Man City ina mabao 78 na ile ya Arsenal inayo 77, Erling Haaland wa City ndiye mchezaji mwenye mabao mengi katika mchezo huu, kwani anayo 32.
Katika safu za ulinzi, City wako vizuri zaidi wakiwa wameruhusu mabao 28 tu na Arsenal 34.
NANI WA KUMZUIA HAALAND?
Katika jamba ambalo mashabiki wa Arsenal wanajiuliza Haaland atazuiwa vipi asifungwe? Hofu huwa kwa mashabiki lakini wachezaji wao wamejipanga bila shaka Mikel Arteta ameandaa kijana wa kutembea na ‘Jini’ ambaye akikufunga anashangilia kwa kukera.
Safu ya ulinzi Arsenal bila shaka itaongozwa na Gabriel Magalhaes ambaye ndiye kinara wa pasi kikosini humo akiwa nazo 2,046 akisaidiwa na Oleksandr Zinchenko aliyerejea kutoka kwenye majeraha, Ben White na golini kama kawa atasimama Aaron Ramsdale mwenye clean sheet 12.
Eneo la kiungo kuna Partey atasimama na pacha wake Granit Xhaka na Bukayo Saka mwenye asisti 11 atakuwa tayari kusambaza pasi za upendo kwa Martinelli mwenye mabao 15 na Gabriel Jesus.
Kama kawa City golini atakuwepo Ederson akipewa sapoti na mabeki Natan Ake na Ruben Dias, Walker na wengineo huku pale kati kama kawa pasi za upendo zitasambazwa na Kevin De Brunye mwenye asisti 15 na ndiye kinara Premier.
Haaland atasimama katikati kusubiri krosi kutoka kwa Mahrez, Jack Grealish pasi za Gundogan pia zinategemewa sana. Kumbuka mara ya mwisho Arsenal kuifunga City Premier ilikuwa mwaka 2015.
ARSENAL KIBOKO, UMEME KAMA KAWA
Licha ya sasa City kuonekana ipo vizuri, ukweli ni kwamba takwimu za jumla zinaibeba Arsenal kwani katika mechi 50 walizokutana, Arsenal wameshinda 23 na City 18 huku wakitoka sare mara 10.
Tangu waanze kukutana Premier, jumla ya kadi nyekundu 13 zimetolewa ambapo Arsenal wamelamba tano na City 8. Kwa upande wa njano City wamepata 105 na Arsenal 79.
Kwa upande wa penalti jumla zimetolewa 12, City kapata saba na Arsenal 5. Wazee wa mkeka mmepata picha ya mkeka wenu?