SIMBA HESABU ZAO KWA WYDAD

AHMED Ally, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba amesema wapo tayari kwa ajili ya mchezo wa robo fainali ya pili dhidi ya Wydad Casablanca.

Mchezo huo unatarajiwa kuchezwa Uwanja wa Mohamed V, nchini Morocco baada ya robo fainali ya kwanza ubao wa Uwanja wa Mkapa kusoma Simba 1-0 Wydad Casablanca.

Ni Ijumaa ya Aprili 28 Simba inatarajiwa kutupa kete yake ya pili na inahitaji ushindi ama kulinda sare kufanikisha malengo ya kutinga hatua ya nusu fainali.

Tayari kikosi kimeanza safari kuelekea Morocco kwa ajili ya mchezo huo na miongoni mwa waliopo ni pamoja na Mzamiru Yassin, Mohamed Hussein,Shomari Kapombe,Ally Salim.

Ally amesema:”Tuna kazi kubwa ya kufanya dhidi ya Wydad mchezo wa robo fainali wachezaji wapo tayari kwa ajili ya kupata matokeo chanya ugenini,”.

Jean Baleke na Henock Inonga ni miongoni mwa wachezaji waliofanya kazi kubwa mchezo wa robo fainali ya kwanza ambapo majina yao yamepenya kwenye kikosi bora cha mchezo wa kwanza wa robo fainali.