SIO Simba wala Yanga kwenye anga za kimataifa hakuna mwenye kazi nyepesi kutokana na mechi zao wote kuwa ngumu katika hatua ya robo fainali.
Kwa mashabiki wakati huu lazima kuungana na kufanya kazi moja kushangalia timu zao huku wachezaji nao akili zao zikiwa kwenye mechi uwanjani.
Kwenye hatua za robo fainali ambacho kinaangaliwa ni ushindi mechi zote mbili bila kujali ni mabao mangapi ila kikubwa ni ushindi wa jumla huu ni muhimu sana.
Kuna wachezaji ambao wanadhani wanakazi nyepesi tofauti na mpinzani kwenye mchezo huo kutokana na aina ya timu ambayo wanakutana nayo.
Hakika hakuna mwenye kazi ndogo, wote wana kazi kubwa na ngumu ndani ya dakika 90 hivyo lazima wajitoe kwa hali na mali kusaka ushindi.
Maneno ni sumu ikiwa hayatafanyiwa kazi kwa vitendo hasa kwa wale ambao wanaamini wana kazi nyepesi ya kupata ushindi kwenye mchezo wao wa robo fainali.
Ushindi nyumbani ni zawadi kwa mashabiki na wapenda mpira kwa kuwa hakuna ambaye atakuwa na furaha akiona timu yake imefungwa ikiwa nyumbani na ugenini ni heshima kuonyesha kwamba inawezekana.
Kasumba ya kuamini kwamba kila mtu ashinde mechi zake bila vitendo hiyo ni mbaya na itawafanya wengi kuondoka uwanjani wakiwa na maumivu matokeo yakiwa tofauti.
Licha ya kuwa kwenye mashindano tofauti bado wote ni wawakilishi wa Tanzania kimataifa Simba kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika na Yanga kwenye Kombe la Shirikisho Afrika.