MGUNDA: BAHATI YAO, YANGA WANGEKULA ZA KUTOSHA

KOCHA Msaidizi wa Simba, Juma Mgunda, ametamba gemu plani yao ndio imewapa matokeo mazuri ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Yanga akisema kwamba ushindi huo ni mdogo kwani kama washambuliaji wao wangekuwa makini, basi Yanga wangekufa nyingi.

Simba juzi ilipata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Yanga katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliochezwa kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.

Ushindi huo umewafanya Simba wafikishe pointi 63 katika msimamo wa Ligi Kuu Bara, huku mabingwa watetezi, Yanga wakiongoza na pointi 68.

Akizungumza na Spoti Xtra, Mgunda alisema katika mchezo huo waliingia kwa gemu plani ya kupata mabao ya mapema yatakayovuruga Yanga na kuwapa presha.

Mgunda alisema kuwa gemu plani hiyo waliianza mazoezini baada ya kuujua udhaifu wa Yanga kutokana na kuwaona katika baadhi ya mechi za Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho Afrika.

Aliongeza kuwa, kama washambuliaji wao Jean Baleke, Kibu Denis na Clatous Chama wangekuwa makini, basi wangepata idadi kubwa ya mabao zaidi ya hayo mawili.

“Umakini mdogo wa washambuliaji wetu ndio umesababisha tuwafunge mabao 2-0, lakini tulikuwa na uwezo wa kuwafunga mabao mengi zaidi ya hayo tuliyoyapata.

“Washambuliaji wetu walipoteza nafasi nyingi za kufunga mabao, hiyo imetokana na gemu plani yetu tuliyoiandaa kufanikiwa kwa asilimia kubwa.

“Tuliwajua vizuri Yanga hasa wachezaji hatari wa kuchungwa katika kikosi chao, hivyo tulihakikisha hatuwapi nafasi ya kucheza, tunashukuru tulifanikiwa katika hilo,” alisema Mgunda.