NASREDDINE Nabi, Kocha Mkuu wa Yanga amesema kuwa kilichowavuruga dhidi ya Simba ni bao la mapema ambalo chanzo chake hakikuwa cha uhakika.
Kwenye mchezo uliochezwa Uwanja wa Mkapa, Aprili 16, ubao wa Uwanja wa Mkapa ulisoma Simba 2-0 Yanga huku bao la kwanza likifungwa na Henock Inonga.
Inonga alipachika bao hilo dakika ya kwanza akitumia krosi ya Shomari Kapombe ambaye alipokea pasi ya Clatous Chama kutoka kwenye miguu ya Saido Ntibanzokiza ambaye alipiga kona ya kwanza kwenye mchezo huo.
Nabi amesema:”Bao la kwanza lilituvuruga hasa ukizingatia kwamba lilitokana na kona ambayo haikuwa kona kwa namna yoyote ile wachezaji walivurugwa na kuanza kujipanga upya.
“Kwa kuwa imeshatokea huwezi kubadili jambo lakini huo ni ukweli wachezaji walijitahidi kufanya vizuri lakini kipindi cha kwanza walikuwa chini hivyo mabadiliko kipindi cha pili yalisaidia angalau kidogo.
“Kwa ushindi ambao wamepata Simba wamestahili kwa kuwa walipambana kuutafuta nasi tutajipanga kwa mechi zijazo,”.
Yanga ni vinara wa ligi wakiwa na pointi 68 wanafuatiwa na Simba wenye pointi 63 wote wamecheza mechi 26.