UONGOZI wa Simba umeweka wazi kuwa kwa sasa umeanza maandalizi kuelekea mchezo wao wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Wydad ambao utachezwa Uwanja wa Mkapa.
Huo ni mchezo wa hatua ya robo fainali Ligi ya Mabingwa ambapo Simba inaipeperusha bendera ya Tanzania kwenye anga hilo.
Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba, Ahmed Ally amesema kuwa wanatambua mchezo huo utakuwa mgumu wanauchukulia kwa uzito na kampeni zitazinduliwa rasmi Aprili 19,2023 Chalinze,Pwani.
“Mechi yetu dhidi ya Wydad AC itakuwa ni Jumamosi Aprili 22, 2023 saa 10:00 jioni. Mnakumbuka mechi za makundi tulicheza saa 1 usiku lakini mechi hii tumepata saa 10 na hilo ni baada ya kuwaomba CAF sababu itakuwa sikukuu ili kila Mwanasimba aje uwanjani.
“Baada ya kumnyoa mtani jana wachezaji walipata muda wa kupumzika na leo wameingia kambini na saa 10 jioni wataanza mazoezi kwenye uwanja wetu wa Mo Simba Arena.
“Kuhusu majeruhi, Kanoute, (Sadio) anasumbuliwa na nyonga na leo atawasili kambini kukutana na madaktari kama atakuwa sawa ataanza mazoezi, hivyo hivyo kwa Aishi Manula atakutana na madaktari kuangalia hali yake.
“Mechi yetu itakuwa na VAR maofisa wake watafika kesho. Wydad AC na wao watafika kesho saa 5 asubuhi wakiwa na msafara wa watu 50 na watakuja na ndege ya kukodi. Waamuzi na wao watafika nchini kesho,”.